Wakati vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vikitarajiwa kuanza hivi karibuni, Kiongozi wa Chama Mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, ameonesha kwa mara nyingine umuhimu wa uzoefu katika kuimarisha demokrasia nchini.
Januari 12, 2026, jijini Dodoma, mwanasiasa huyo mkongwe ametoa mafunzo maalumu kwa wabunge wa chama hicho, hatua inayotafsiriwa kama uwekezaji mkubwa katika akili za vijana wanaoingia bungeni.
Mafunzo haya si tu semina ya kawaida, bali ni "darasa la kiungwana" lililolenga kuwanoa wabunge, hususan wale vijana, ili waweze kumudu mikiki ya kibunge kwa weledi, hoja, na kufuata misingi ya kisheria.
Katika mifumo ya kibunge duniani, wabunge wa upande wa wachache (Minority) wana jukumu zito la kuwa "macho na masikio" ya wananchi. Faida kubwa ya mafunzo haya kwa wabunge vijana ni kuwapa ujasiri (confidence) wa kusimama bungeni bila kutetereka.
Wanajifunza namna ya kuchambua bajeti, kuhoji matumizi ya serikali kwa kutumia takwimu, na kuwasilisha kero za wananchi kwa lugha ya staha lakini yenye shinikizo la kisheria.
Zitto Kabwe, akiwa mwanasiasa aliyebobea katika usimamizi wa rasilimali na utawala bora, anawarithisha vijana hawa mbinu za "kuamsha" serikali. Jukumu la upinzani ndani ya bunge si kupinga kila kitu, bali ni kuishauri na kuiwajibisha serikali ili kuhakikisha huduma za jamii zinawafikia walengwa.
Kwanini Zitto Anawaandaa?
Zitto anafanya kazi hii ya maana kwa sababu anatambua kuwa bunge imara linahitaji wabunge walioandaliwa vyema. Katika siasa za kisasa, hoja haijibiwi kwa matusi, bali kwa hoja mbadala. Kwa kuwanoa vijana hawa, anahakikisha kuwa chama chake kinaingia bungeni kikiwa na "makucha" ya kisheria na kitaalamu.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu, Mbarala Maharagande, imebainisha kuwa mafunzo haya yanalenga kuifanya ACT Wazalendo kuwa sauti ya kweli ya wananchi. Hii inasaidia kukuza ukomavu wa demokrasia ambapo serikali inapata changamoto chanya inayopelekea utendaji bora zaidi.
Semina hii imejikita katika mchakato wa utungaji wa sheria na usimamizi wa serikali. Kwa vijana wanaoingia bungeni, uzoefu wa Zitto unawasaidia kufupisha safari ya kujifunza kwa vitendo (learning curve). Badala ya kupoteza muda mwingi kujifunza kanuni za bunge wakiwa ndani ya ukumbi, wanatoka kwenye mafunzo haya wakiwa tayari kupangua hoja .
Mkakati huu wa ACT Wazalendo unakumbusha umuhimu wa taasisi za siasa kuwekeza katika watu wao. Taifa linanufaika pale ambapo upande wa wachache unapokuwa na wabunge wenye uwezo wa kuchambua dira za nchi kama Dira ya 2050 na kuhakikisha utekelezaji wake unazingatia haki na usawa.
Mwisho wa siku, bunge lenye wabunge walioiva kifikra ndilo bunge linaloweza kuivusha Tanzania kuelekea maendeleo ya kweli yenye maslahi mapana ya Taifa.

0 Comments