DIPLOMASIA YA SAMIA YAZIDI KUNG’ARA: MATAIFA YASAKA FURSA ZA USHIRIKIANO TANZANIA

Ufanisi wa diplomasia ya uchumi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umezidi kudhihirika kufuatia mataifa mbalimbali duniani kuonyesha nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika nyanja za kimkakati. 

Hatua hii ni mwendelezo wa imani ambayo jumuiya ya kimataifa imekuwa nayo kwa Tanzania kutokana na utulivu wa kisiasa na mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara yaliyowekwa na serikali.

Katika kuelekea mapinduzi ya kijani jijini Dodoma Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo amefanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tone Tinnes ambapo walijadili mikakati mipya ya ushirikiano katika sekta ya kilimo.

Mazungumzo hayo yamejikita zaidi katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kilimo inayolenga kuongeza tija katika uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima wadogo nchini. Norway imeonekana kuwa mshirika muhimu katika kuleta ujuzi wa kiteknolojia utakaosaidia wakulima wa Tanzania kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza thamani ya mazao yao kwa ajili ya soko la ndani na nje.

Wakati hayo yakijiri katika sekta ya kilimo huko jijini Riyadh nchini Saudi Arabia Tanzania na Serbia zimeingia katika hatua nyingine ya ushirikiano wa kimaendeleo. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano ,Deus Sangu na Waziri wa Kazi wa Serbia, Milica Djurdjevic Stamenkovski wamekutana na kujadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kazi na maendeleo ya rasilimaliwatu. Serbia imeonyesha nia ya kutaka kunufaika na nguvu kazi ya Tanzania hususan katika sekta ya ujenzi na maeneo mengine muhimu ya kiuchumi kutokana na sifa bora ya wafanyakazi wa kitanzania duniani.

Waziri Sangu amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania imeendelea kufanya mageuzi makubwa yanayolenga kukuza ajira zenye staha na kuongeza ujuzi kwa nguvu kazi ya taifa. 

Ametumia jukwaa hilo kueleza uwezo mkubwa wa wataalamu wa kitanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo uhandisi afya TEHAMA uhasibu na utalii. Sifa kuu za watanzania ambazo ni bidii unyenyekevu na maadili mema kazini zimetajwa kuwa kivutio kikubwa kwa mataifa ya Ulaya kama Serbia kuanza kuajiri watanzania kwa wingi.

Kama kielelezo cha kukubalika kwa Tanzania Waziri Milica wa Serbia amebainisha kuwa nchi yake ipo katika mchakato wa kufungua ubalozi nchini Tanzania ili kurahisisha na kukuza ushirikiano huo wa kidiplomasia na kiuchumi. 

Hatua hii inatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ni ushindi mwingine wa diplomasia ya Tanzania inayolenga kutafuta fursa za ajira na masoko ya bidhaa za kitanzania duniani kote. Kwa hakika mataifa ya duniani sasa yanaitazama Tanzania kama mdau muhimu wa kimaendeleo jambo linalochochea kasi ya kukua kwa uchumi wa taifa na maendeleo ya watu wake.

Post a Comment

0 Comments