Na Beda Msimbe, BSKY Media
Mwenendo wa uchumi wa Tanzania unaendelea kupata msukumo mpya kutokana na mageuzi makubwa ya kiutendaji yanayofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameweka wazi kuwa wastani wa makusanyo kwa mwezi katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 umefikia Shilingi Trilioni 3.13, ikiwa ni ongezeko kubwa la asilimia 107 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Trilioni 1.51 kilichokuwa kikikusanywa kabla ya uongozi wa sasa.
Katika kudhihirisha kukua kwa nidhamu ya ulipaji kodi kwa hiari, mwezi Desemba 2025 pekee, TRA imeweza kuvunja rekodi kwa kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 4.13, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 15.5 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Ndugu Msigwa alisema hayo baada ya kukamilisha kutembelea bandari ya Dar es salaam akiwa na waandishi wa habari na kuwa na mkutano wao kuelezea mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita katika kuboresha bandari na tija kuonekana.
Alisema pia ili kuendeleza kasi hii ya makusanyo na kuondoa kero kwa wafanyabiashara, Serikali inatarajia kuzindua rasmi Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani unaojulikana kama IDRAS ifikapo tarehe 9 Februari, 2026.
Mfumo huu wa kisasa utaleta mapinduzi makubwa kwani utawawezesha walipakodi kupata huduma masaa 24 kwa siku saba za wiki bila kuhitaji kufika ofisi za TRA, ikiwemo kutoa risiti za kielektroniki bure kwa njia ya mtandao na kufuatilia maombi ya hati za ulipaji kodi kiotomatiki.
Aidha, mfumo wa IDRAS utakuwa na uwezo wa kusomana na mifumo ya taasisi nyingine za serikali kwa ajili ya kubadilishana taarifa, jambo litakalopunguza usumbufu kwa wananchi, kuongeza uwazi katika makusanyo ya kodi za PAYE kwa waajiriwa, na kuepusha adhabu na migogoro isiyo ya lazima kupitia vikumbusho vya kiotomatiki.
Ndugu Msigwa alisema lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuwa na mfumo mmoja jumuishi ambao unalenga kwenda kusaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji kodi na kulinda haki za walipakodi, kwani utasaidia pia katika utunzaji wa kumbukumbu.
Msigwa alisema mfumo huo wa kisasa, utaongeza ufanisi, utaleta usawa na kuondoa usumbufu kwa sababu up utajumuisha huduma zote zilizokuwa zinatolewa
katika mifumo ya TRA ikiwemo usajili wa walipakodi, utumiaji wa taarifa zote za kodi, ulipaji wa kodi, mawasiliano na madai mbalimbali kuendana na kauli ya
mamlaka hiyo ya kwenda kuboresha huduma kwa walipakodi na kuwataka watanznaia walipe kodi kwa maendeleo ya taifa lao.
Ndugu msigw aalisema kwamba mfumo unakwenda kutenda haki kwa walipakodi, kwa sababu utakuwa na taarifa nyingi ambazo zitatoa makadirio sahihi lakini utaungana na mifumo mingine kwani ina uwezo wa kuungana na mifumo 500.

0 Comments