Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, imetembelea Gereza Kuu la Arusha kusikiliza ushahidi wa makundi mbalimbali.
Akiwa gerezani hapo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, amefanya mazungumzo na uongozi wa gereza pamoja na mahabusu 10 waliosalia gerezani humo kutokana na matukio hayo.
Mahabusu hao, wakiwemo wanaume kenda (9) na mwanamke mmoja (1), wanatarajiwa kufikishwa mahakamani tena Januari 14, 2026.
Jaji Mstaafu Chande amebainisha kuwa lengo la tume hiyo ni kuzungumza na wahusika na waathirika wa makundi yote ili kubaini kiini cha machafuko hayo na kutoa mapendekezo yatakayozuia matukio kama hayo kujirudia katika mustakabali wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu Arusha, Vicent Karani, ameitaarifu tume hiyo kuwa awali walipokea jumla ya mahabusu 197 waliohusishwa na vurugu za uchaguzi. Hata hivyo, mahabusu 187 tayari wameachiwa huru na mahakama, huku 10 waliosalia wakikabiliwa na kosa la pili la nyongeza.
Tume hiyo inaendelea na ziara zake katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya kuhoji waathirika na kukusanya taarifa kamili kabla ya kuwasilisha ripoti rasmi kwa mamlaka husika.


0 Comments