JINSI MELI ZA KITALII ZINAVYONOGESHA AJIRA NA KIPATO CHA MTANZANIA

Utalii wa meli sasa umeanza kuleta neema ya moja kwa moja kwenye mifuko ya Watanzania! Hivi karibuni, meli ya kifahari ya Crystal Symphony imetia nanga jijini Dar es Salaam ikiwa na watalii zaidi ya 500, tukio ambalo ni zaidi ya kutembelea vivutio—ni mzunguko wa fedha unaogusa kila sekta.

Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ernest Mwamwaja, amebainisha kuwa ushirikiano kati ya TTB na Mamlaka ya Bandari (TPA) unalenga kuitangaza Tanzania kama kitovu kikuu cha utalii wa majini, huku shabaha ikiwa ni kufikia watalii milioni nane.

Meli moja inapotia nanga, mnyororo wa thamani unamfikia kila mtu. Hivi ndivyo watalii hawa 500 wanavyochochea ajira:

Sekta ya Usafirishaji: 

Madereva wa teksi, Uber, na mabasi ya utalii wanapata abiria wa uhakika kuwapeleka maeneo kama Hifadhi ya Nyerere na Bagamoyo.

Wajasiriamali na Wasanii: 

Maeneo kama Soko la Samaki Ferry, Kijiji cha Makumbusho, na vituo vya kazi za mikono yanachangamka. Watalii hununua vinyago, batiki, na bidhaa za kitamaduni, jambo linaloingiza fedha mbichi kwa msanii wa mtaani.

Waongoza Watalii (Tour Guides): 

Vijana wengi wanapata ajira za muda mfupi na msimu (seasonal jobs) kufanya mathalani utoaji wa maelezo kwenye maeneo ya kihistoria kama Kanisa la Mtakatifu Joseph na Makumbusho ya Taifa.

Mama Lishe na Migahawa: 

Watalii wanapotoka nje ya meli, wanataka kuonja ladha ya vyakula vya kitanzania. Hii ni fursa kwa migahawa ya ndani na watoa huduma za vyakula kunufaika.

Kwa upande wa Serikali, utalii huu ni mgodi wa dhahabu wakati kwa  Mamlaka ya Bandarii (TPA): Kupitia tozo za meli kutia nanga na huduma za bandarini wanaingiza kipato.

Kila mtalii anapotumia dola yake nchini, anaongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya shilingi. Huku kwa wao kutembelea maeneo kama Hifadhi ya Nyerere na Kisiwa cha Mbudya kunaongeza mapato ya moja kwa moja kwenye mfuko wa hazina kupitia TANAPA na mamlaka nyingine.

Katika kuimarisha uhusiano, TTB ilimkabidhi zawadi Nahodha wa meli hiyo, Tonci Hladilo, ikiwa ni ishara ya ukarimu. Hii si zawadi tu, bali ni mkakati wa kumfanya nahodha huyo awe balozi wetu huko nje, ili alete meli nyingi zaidi nchini.

Utalii wa meli ni uchumi wa papo kwa hapo. Meli ikikaa bandarini kwa saa 24, mamilioni ya shilingi yanaingia mtaani. Tunapaswa kuboresha zaidi miundombinu yetu ya majini na kuwa na bidhaa nyingi za kitamaduni karibu na bandari ili mnyororo huu wa ajira na kipato usikatike.

Post a Comment

0 Comments