VIJANA TUSIHUKUMU TUPAMBANE KWANI UTAJIRI SI MILIKI YA VITU NI MILIKIYA AKILI

Katika ulimwengu wa leo wa "Snapchat" na "Instagram," ambapo kila mtu anajaribu kuonekana ana mafanikio kwa kumiliki iPhone ya hivi karibuni au kupiga picha pembeni ya gari la kifahari, mfanyabiashara Lucy Oisso ameturudisha kwenye mstari kwa maneno mazito: "Utajiri wa mtu si wingi wa vitu alivyonavyo, bali ni namna gani anafikiri kufikia malengo yake."

Huu ni ujumbe wa kishindo kwa kila kijana anayetafuta utajiri wa haraka bila kujenga msingi wa maarifa. Lakini, kwa nini ndoto za wengi zinakufa zikiwa changa?

Oisso akizungumza na vijana wenzaqke kwa kutumia njia ya televisheni anabainisha changamoto kubwa inayozunguka kwa vijana: Chuki dhidi ya waliofanikiwa. Vijana wengi, badala ya kusogea karibu na kujifunza, hukaa pembeni na kuhukumu wakisema kuwa 'yule amepata kwa njia zisizo sahihi' au 'ana nyota ya ajabu.'

Ukweli ni kwamba, huwezi kuvuna matunda ya mti uliouchukia. Kama unataka kuwa tajiri, lazima upende matajiri na uwe tayari kukaa chini yao ufundishwe. Mafanikio yana ramani na ramani hiyo inashikiliwa na wale waliotangulia.

Kwenye mitandao ya kijamii, mjadala huu umepamba moto, na hapa kuna hoja chache zenye "punch" ambazo vijana wamezitoa.

 Mdau mmoja amepigilia msumari kwa kusema: "Utajiri ni mali na pesa zinazokutumikia wewe, siyo unazozitumikia." Ukiwa na gari zuri lakini unashinda unawaza jinsi ya kupata hela ya mafuta na service, wewe hujaumiliki utajiri—utajiri umekumiliki wewe!

Wengine wamecheka tabia ya vijana kujiita Ma-CEO kwenye Bio za Instagram wakati biashara zao hazina hata anuani ya makazi (Digital Address). Utajiri wa kweli hauhitaji Antenna za kujionyesha; unajengwa kimya kimya kupitia mifumo na teknolojia.

Kwa kijana unayechipukia, hekima ya Oisso inakupa mambo matatu ya kuondoka nayo , kwamba ni vyema ukabadili fikira yaani 'Mindset' maana yake acha kuwaza kununua iPhone ya milioni 3 wakati mtaji wa biashara yako ni laki 5. Fikiria jinsi ya kuifanya ile laki 5 izae pesa itakayokununulia simu hiyo baadaye bila kutikisa mtaji.

Pia maelezo yake  yanashawishi kijana asiwe na aibu kuuliza. Kaa na watu waliofanikiwa, sikiliza hadithi zao za kufeli, na ujifunze mbinu zao za ushindi.

Kwa kuwa Dira ya 2050, uchumi utatawaliwa na maarifa na teknolojia, fursa zinahitaji akili inayofikiri, siyo mikono inayobeba vitu pekee.

Kama wasomi wanavyosema,mafanikio ni matokeo ya kile kilichobaki kichwani mwako,utajiri wa kweli huanzia kwenye uwezo wako wa kutatua matatizo ya watu kwa kutumia teknolojia na ubunifu. Ukishatatua shida za watu, pesa zitakufuata na kuanza kukutumikia.

Post a Comment

0 Comments