Wakati mwingine vijana tunapoteza muda mwingi kwenye malumbano yasiyo na tija, huku ramani ya utajiri wa nchi yetu ikichorwa upya mkoani Mtwara. Katika kitalu cha Mnazi Bay, maandalizi ya kuchimba visima vitatu vipya vya gesi asilia yamefikia asilimia 90 hadi kufikia Februari 3, 2026. Huu ni ujumbe tosha kwa kizazi kinachotafuta mwelekeo; nchi imeshasimika mitambo ya mafanikio, kazi imebaki kwako kukamata fursa.
Mhandisi Felista Ndabita kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) amethibitisha kuwa mtambo wa uchorongaji (Rig) umeshasimikwa na uko tayari kuanza kazi. Kwa sasa, kitalu hicho tayari kinazalisha wastani wa futi za ujazo milioni 90 hadi 100 kwa siku kupitia visima vitano vilivyopo.
Lakini visima hivi vitatu vipya siyo tu habari ya nishati, ni injini ya uchumi kwa vijana wenye macho ya mbali kwani gesi hii itatumika kuzalisha umeme na kuendesha viwanda vikubwa, ambavyo ni vyanzo vikuu vya ajira.
Aidha ongezeko la uzalishaji litashusha gharama za nishati kwenye magari na majumbani, ikifungua milango kwa mafundi na wasambazaji wa vifaa vya gesi.
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeridhishwa na kasi ya mradi huu, ikihakikisha kuwa malengo ya Taifa yanafikiwa.
Hata hivyo, utajiri huu wa gesi hautakuja kukufuata kijiweni kama hutakuwa umechoshwa na maisha ya kawaida na kulalamika kuhusu ajira za maofisini, sekta ya gesi inahitaji watu wenye ujuzi, watoa huduma, na wajasiriamali wanaoweza kwenda na kasi ya teknolojia.
Kama wasemavyo wadau, "Let's change Africa to the top." Gesi ya Mnazi Bay ni uthibitisho kuwa Tanzania ni nchi yenye baraka za kipekee. Kijana, muda wa malumbano umepita; mitambo imeshasimikwa Mtwara—je, upo tayari kuwa sehemu ya mnyororo huu wa thamani?

0 Comments