Rais Samia ameweka mchoro, sasa kazi imebaki kwa vijana wenyewe

Bunge la 13 limefanya uchambuzi wa hotuba ya kihistoria ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 14, 2025. Safari hii, wabunge hawakujadili namba pekee, bali walijadili "uhalisia wa maono." 

Kuna watu wanajilalamikia tu bila kufikiri kama nyumbu  kwamba wabunge walikuwa wanafanya uchawa, sio suala la 'uchawa' au sifa zisizo na msingi, bali ni kutambua ukweli wa mwelekeo mpya ambao Rais ameuweka kwa ajili ya mustakabali wa asilimia 60 ya Watanzania—ambao ni vijana.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni mageuzi makubwa ya kiuongozi, Rais Samia amevunja ukimya na kutekeleza ahadi yake ya kuunda Wizara kamili ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais. Hatua hii imepokelewa kwa 'tano' na wabunge, wakibainisha kuwa kuiondoa idara ya vijana kutoka kwenye wizara zilizosongwa na majukumu mengi ni kumpa kijana sauti, mamlaka, na jukwaa rasmi la kushughulikia changamoto zake, hususan ukosefu wa ajira na mitaji.

Wabunge, akiwemo Dk. Emmanuel Nuwa wa Mbulu na Hawa Chakoma wa Viti Maalum, wamethibitisha bungeni kuwa maono haya yameshaanza kuzaa matunda kwa vitendo. Tayari mabilioni ya fedha yameshaanza kutiririka; Shilingi bilioni 10.5 zimepelekwa Benki ya NMB kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu ya asilimia saba, huku Rais akiahidi jumla ya Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kiuchumi za vijana na wanawake. Huu ni ujumbe mzito kwa vijana kuwa "muda wa kulalamika umekwisha, sasa ni wakati wa kuchangamkia fursa."

Mjadala huo bungeni umeweka wazi kuwa ufunguo wa maendeleo ya kijana hautategemea tena 'mikopo umiza' au majukwaa ya kisiasa yaliyopoteza mvuto, bali utategemea sera madhubuti na programu za kimkakati. 

Wabunge wamehimiza kuwa wizara hii mpya iwe mhimili wa kuunganisha vijana na sekta za kilimo, madini, na teknolojia ya habari.

Mbunge Agnesta Lambert amesisitiza kuwa hotuba ya Rais imekidhi matakwa ya wananchi wote bila kujali itikadi, akiamini kuwa utawala bora na uwajibikaji ndio utakaofanya matamanio ya Rais yatekelezwe mitaani.

Bunge pia limefanya vyema kwa kutoa rai kwa watendaji na viongozi waliopewa dhamana kuhakikisha "fyekeo" la Rais linafanya kazi kwa wale watakaochelewesha au kukwamisha fedha hizi kuwafikia walengwa. 

Kwa uundwaji wa Baraza la Vijana na uimarishaji wa mifuko ya maendeleo, Tanzania inajipanga kuhakikisha nguvu kazi yake kubwa haipotei kwanye vurugu, bali inageuzwa kuwa injini ya uchumi kuelekea Dira ya 2050. 

Ni dhahiri kuwa Rais Samia ameweka mchoro, na sasa kazi imebaki kwa vijana wenyewe "kukaa mkao wa kula" na kutumia zana zao, ikiwemo teknolojia, kutafuta na kutumia fursa hizi adimu.

Post a Comment

0 Comments