SIMULIZI YA MAPINDUZI YA AFYA YA UZAZI LINDI INAVYOTAMANISHA KUZAA TENA


"Natamani kuendelea kuzaa watoto wengine zaidi kwa hili lililotokea katika huduma za afya, japo tayari nina mjukuu!” Hii ni kauli ya kusisimua ya Vumili Mohammed, mkazi wa Kijiji cha Kuchochorokana, wilayani Liwale mkoani Lindi.

Vumili, ambaye binti yake Sharuu Iddi amejifungua hivi karibuni, anasimulia kwa tabasamu kubwa namna ambavyo hivi sasa mwanamke anafika kituo cha afya akiwa na nguo zake tu, na kukuta kila kifaa kinachohitajika kikiwa tayari na bure kabisa. Hii ni tofauti kubwa na zamani ambapo wazazi walipaswa kuandaa orodha ndefu ya vifaa, na mara nyingine kukataliwa huduma wasipokuwa navyo.

Mabadiliko haya katika eneo hili  ni matokeo ya muungano wa Serikali na Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).Mwaka 2023, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na shirika la MSF  imeweka kambi wilayani Liwale kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto. Mradi huu unatekelezwa katika zahanati tatu, vituo vya afya viwili, na Hospitali ya Wilaya ya Liwale.

Matokeo ya ushirikiano huu idadi ya wanaojifungulia hospitali imeongezeka kutoka wanawake 9,324 (mwaka 2020) hadi kufikia 12,059 (mwaka 2025).Aidha vifo vya uzazi vimepungua kwa kasi ya ajabu kutoka vifo 119 hadi kufikia vifo 16 tu tangu mradi uanze.

Mabadiliko haya hayakuishia kwenye vifaa tu, bali yameingia mpaka kwenye fikra za watu. Sakina Saidi, mkazi mwingine wa Liwale, anasema huko nyuma watoto walipopata degedege walikimbizwa kwa waganga wa kienyeji wakiamini dawa za hospitali "hazipatani" na ugonjwa huo.

“Sasa tunawapeleka hospitali na wanapona,” anasema Sakina, akishukuru elimu inayotolewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs). Wahudumu hawa, wakiongozwa na Said Hassan, wameunda hadi 'Mother Clubs' (Klabu za Akina Mama) na kutembelea nyumba kwa nyumba kutoa elimu ya lishe, usafi, na unyonyeshaji.

Meneja Mradi wa MSF, Azhar Shah, anabainisha kuwa moja ya siri ya mafanikio haya ni kuwajengea morali watumishi. MSF inatoa asilimia 30 ya mishahara kwa wafanyakazi wa Serikali katika Hospitali ya Liwale ili kuwavutia wabaki na wafanye kazi kwa moyo, kwani maeneo mengi ya wilaya hiyo ni vigumu kufikika.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Hadija Kitiku, na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Hamisi Namaleche, wamepongeza juhudi hizo wakisema zimesaidia si tu kwenye vifaa na watumishi, bali hata kutoa mahitaji ya kijamii kama taulo za kike na vifaa vya shule kwa watoto.

Leo hii, Liwale si tena mahali pa hofu kwa mjamzito, bali ni mfano wa namna ushirikiano kati ya Serikali na wadau unavyoweza kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Post a Comment

0 Comments