Wiki hii, taswira ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akipokea nakala ya kitabu "Jamhuri ya Plato" kutoka kwa Bw. Walter Bgoya wa kampuni ya Mkuki na Nyota, imeamsha mjadala mzito wa kifikra.
Kitabu hiki si kingine bali ni tafsiri adhimu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetafsiri kazi ya mwanafalsafa Plato, The Republic.
Lakini, kwanini kijana wa leo anayeishi kwenye ulimwengu wa 'TikTok' na 'Digital Economy' akihitaji kitabu hiki? Na kwanini viongozi wetu wanapaswa kuonja "utamu" wa falsafa hii?
Katika ulimwengu wa sasa uliotawaliwa na siasa za upotoshaji (populism) na kelele za mitandaoni, Jamhuri na Plato ni dira. Mwalimu alikitafsiri ili kijana wa Kitanzania asome falsafa hiyo kwa lugha yake ya Kiswahili—lugha inayobeba utu wake kwani ndani ya kitabu hicho kuna siri ya kuwa raia wa kisasa (Si mshabiki tu).
Plato kwa kuujadili Mji Bora (Kallipolis) anafundisha vijana kuelewa wajibu wako kama raia, si tu kulalamika, bali kushiriki kujenga jamii yenye usawa kwa kuzingatia nidhamu ya nafsi.Plato anasema mji hauwezi kuwa na amani kama nafsi za watu wake hazina kiasi. Kijana anayejitambua ni yule anayeweza kutawala tamaa zake kabla ya kutafuta kutawala wengine.
Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa uongozi wa hekima . Alitafsiri kitabu hiki kwa sababu aliona Afrika inahitaji "Wanafalsafa-Wafalme"—viongozi ambao si tu wana amri, bali wana maarifa, maadili, na hofu ya dhuluma. Katika karne ya 21 ya siasa za ubinafsi, Plato anatukumbusha kuwa mtawala ni mlinzi wa maslahi ya wote.
Mwalimu hakukitafsiri kama zoezi la kitaaluma. Alikifanya kama hitaji la msingi la kifikra. Alitaka Watanzania wawe na uwezo wa kutafakari masuala mazito ya utawala, asili ya nafsi, na nadharia ya maumbo kwa lugha yao wenyewe.
Tafsiri ya Mwalimu Nyerere ni zawadi ya mwisho ya kifikra kwetu. Inatuachia swali moja kubwa la kutafakari: Je, tunajenga jamii inayothamini hekima, au tunajenga jamii inayofurahia vurugu ?

0 Comments