Moshi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya imetembelea na kukagua Makazi ya Wazee yanayomilikiwa na Serikali yaliyopo Njiro Mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kuona hali ya huduma zinazotolewa kwa wazee wanaoishi katika kituo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Hawa Mchafu ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa juhudi inazozifanya kuhakikisha wazee wanapata huduma katika vituo mbalimbali nchini.
“Tunawapongeza Wizara kwa hatua hii ya kuwahudumia wazee katika makazi maalum ni jambo la muhimu kwa ustawi wa jamii, hasa kwa wazee wasiokuwa na msaada wa familia hivyo ni jukumu letu kuendelea kulisemea bungeni kwaajili ya kuendelea kuboresha maisha ya wazee wote Nchini. Ni jambo jema na baraka kutoka kwa Mungu hivyo tutaendelea kuliwekea mkazo suala hili la wazee na kuja kuwaona na ikiwezekana tuwaalike na wadau waweze kuongeza kunguvu ili mahitaji muhimu yaweyanapatikana kwa wakati." amesema Mhe. Mchafu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, amesema Wizara inaendelea kusisitiza umuhimu wa familia kutunza na kuwalea wazee wao kama sehemu ya maadili ya jamii ya Kitanzania ambapo Serikali inaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwalea wazee wanaokosa msaada wa familia pale inapobidi.
“Tunasisitiza jamii na familia kufanya malezi sahihi kwa wazee wao Serikali inatimiza wajibu wake kwa kuwalea wazee hawa, pale ambapo kila kitu kimeshindikana lakini pia tumepokea pia maelekezo ya Kamati kuhusu maboresho ya kituo hiki na tutayafanyia kazi,” amesema Mhe. Mahundi.
Nao baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameitaka Wizara kuendelea kusimamia malezi na huduma zinazotolewa kwa wazee katika vituo hivyo pamoja na kuongeza vifaa na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wanaowahudumia wazee, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
0 Comments