Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi ameungana na Mkurugenzi wa Child Support, Noela Msuya kutembelea na kutoa msaada wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia Shule ya watoto wenye ulemavu Katumba 2 iliyopo Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Mhandisi Maryprisca ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Maryprisca Women Empowerment Foundation (MWEF) amesema kupitia Taasisi hiyo atajitahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu.
Aidha hakusita kumpongeza Noela Msuya kwa namna anavyojitolea na kuwagusa watoto wenye mahitaji maalumu.
Katika ziara hiyo Mh Mhandisi Maryprisca aliambatana na Mbunge wa Viti Maalumu Zanzibar, Nassir Ally ambaye aliguswa kwa namna Maryprisca anavyouagusa makundi yenye uhitaji ambapo ameahidi kurudi Kituo hicho ili kujifunza zaidi namna wanavyowahudumia watoto wenye ulemavu.
Amesema wadau wengine wajifunze kupitia Noela Msuya kwa sababu Serikali haiwezi kufanya kila jambo hivyo aendelee na moyo huo huo.
Kwa upande wake Noela amesema kupitia Child Support ameweza kukarabati miundombinu ya shule hiyo ili kuwaondolea vikwazo watoto wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine Noela Msuya ametoa Viti mwendo zaidi ya kumi,mafuta kwa watoto wenye ualbino, kutoa mafunzo kwa walimu, kuanzisha klabu ya ulinzi kwa watoto na klabu ya Wazazi.
Pia Noela amekabidhi vifaa vya kusomea kwa watoto wenye uoni hafifu panoja na mpango mkakati kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu ameshukuru kupokea msaada huo kwa watoto wenye ulemavu kwani itasaidia kutatua baadhi ya changamoto.
Shule ya Katumba ni shule jumuishi inayopokea watoto wasio na ulemavu na wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali nchini.









0 Comments