AMANI KWANZA: WANANCHI WA SHINYANGA WAWASIHI VIJANA KULINDA UTANGAMANO WA TAIFA


 Wakazi wa Kata ya Solwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wametoa wito mzito kwa vijana kuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha amani, wakisisitiza kuwa ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walibainisha kuwa sekta muhimu kama elimu, biashara, uwekezaji na michezo haziwezi kustawi bila kuwepo kwa utulivu na usalama.

"Vijana ndio nguvukazi ya taifa. Wanapaswa kuelekeza nguvu na akili zao kwenye shughuli za uzalishaji mali, masomo na michezo, badala ya kujiingiza kwenye migogoro, uhalifu au matumizi ya dawa za kulevya," alisema mmoja wa wakazi hao.

Katika hatua nyingine, wananchi hao walipongeza kwa dhati mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026. Walieleza kuwa mashindano hayo yamekuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha vijana kutoka maeneo mbalimbali, huku yakiwajenga katika misingi ya mshikamano, upendo na kuishi kwa amani.

Mwishoni, walitoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuacha misingi ya utengano na badala yake wadumishe umoja na ushirikiano ili kuijengea nchi mazingira salama na bora kwa kizazi cha sasa na vile vijavyo.

Post a Comment

0 Comments