Vijana nchini wameonywa kutokubali kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kufuata matamko ya uchochezi na chuki yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, huku wale wanaowahamasisha kufanya fujo wakibaki salama na familia zao.
Onyo hilo limetolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, wakati akizundua Shina la Wakereketwa wa Bajaji na Bodaboda Stendi ya Sanya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Alisisitiza kuwa hakuna mafanikio yanayopatikana kwa kufuata mkumbo wa maneno ya kisiasa yasiyolenga kuboresha maisha ya wananchi, na akawataka vijana kutanguliza kazi na uzalishaji mali badala ya kushawishiwa kushiriki vitendo vinavyoweza kuathiri na kuharibu kabisa mstakabali wa maisha yao ya baadaye.
Katika hotuba yake, Kihongosi alikumbusha kuwa maisha ya kila siku yanategemea nguvu ya mtu mwenyewe na si vyama vya siasa, akitoa mwongozo kuwa akili ya kuambiwa ni vyema ichanganywe na ya kwako mwenyewe ili kuepuka kubebwa na mahaba yanayopotosha.
Aliwasihi vijana kutumia viongozi wao wa kuchaguliwa kuwasilisha changamoto zinazowakabili badala ya kukata tamaa au kuingia barabarani, kwani viongozi wanaowajibika wapo kwa ajili ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi sahihi.
Alibainisha kuwa mazingira salama na ya amani ndiyo yanayotoa nafasi kwa vijana kujitafutia mkate wa kila siku na kujenga uchumi wao bila kuingizwa kwenye migogoro isiyo na tija.
Awali, Mbunge wa Hai, Saashisha Mafue, aliiomba CCM kusaidia kusukuma utekelezaji wa utoaji wa mikopoya asilimia kumi kwa makundi ya bodaboda, akieleza kuwa vijana hao wameonyesha utayari wa kujiunga katika vikundi na kunufaika na fedha zinazotengwa kwa mujibu wa utaratibu wa halmashauri.
Mafue amesema utekelezaji wa mikopo hiyo utasaidia kuongeza uwezo wa vijana kujiajiri, kukuza uchumi wa kaya zao na kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Hai kwa ujumla.
Akisoma taarifa ya shina hilo lenye jumla ya wanachama 78 wakiwemo waendesha bajaji 39 na bodaboda 39, Mwenyekiti Joseph Massawe alieleza kuwa lengo lao kubwa ni kuhamasisha shughuli za maendeleo. Hata hivyo, alibainisha changamoto kubwa inayowakabili kuwa ni kutomiliki vyombo hivyo wanavyovifanyia kazi, hali inayowalazimu kutumia sehemu kubwa ya mapato yao kulipa wamiliki.
Kutokana na changamoto hiyo, Massawe aliiomba Serikali kuwasaidia kupata mikopo nafuu ya pikipiki na bajaji ili waweze kujitegemea kiuchumi, huku wakiahidi kuendelea kuwa wazalendo, kukitetea chama na kujiepusha na vishawishi vyote vya uvunjifu wa amani.

0 Comments