SANGU: WALIOFUJA FEDHA ZA SHULE MFINGA WAFIKISHWE MAHAKAMANI

 

Na: Mwandishi Maalumu, Kwela

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ametaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mheshimiwa Ephraim Konta kufuatilia kwa karibu jalada la uchunguzi la ujenzi wa Shule ya Msingi Mfinga lililopo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili hatua stahiki zichukuliwe na wahusika wa ubadhirifu wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

Waziri Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela ambapo shule hiyo ipo, ameeleza kuwa Serikali ilitoa shilingi milioni 220.1 kwa mradi huo tangu Julai 2025, lakini mpaka sasa ujenzi bado haujakamilika jambo ambalo linaibua maswali kuhusu uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mradi huo mpaka sasa tayari umetumia Shilingi milioni 212.9.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mfinga Chrispin Costantino Ismail amesema fedha za mradi huo zililenga kujenga vyumba viwili vya madarasa ya elimu ya awali, vyumba sita vya madarasa ya shule ya msingi, matundu sita ya vyoo pamoja na uzio wa shule na kwamba mradi ulipaswa kukamilika Novemba 2025 lakini hadi sasa haujakamilika huku zikiwa zimebaki shilingi milioni 7.1 pekee.

Akizungumza Julai 19, 2026 baada ya kukagua mradi huo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kuhamasisha shughuli za maendeleo katika Jimbo la Kwela, Waziri Sangu alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo licha ya fedha nyingi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.

“Fedha hizi zililetwa na Serikali kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto. Leo tunaelezwa na Mkaguzi wa Ndani kuwa mradi una hasara ya shilingi milioni 40. Siwezi kukubaliana na hali hii wakati waliohusika bado wako mitaani bila kuchukuliwa hatua,” alisema Sangu mbele ya wananchi.

Waziri Sangu alisema baada ya ukaguzi kwamba kuna viashiria vya wazi vya matumizi mabaya ya fedha za umma na kutaka watumishi wa umma wote wanaodaiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Mfinga kufikishwa mahakamani haraka.

Mbunge huyo amesema amepokea taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya watu walikuwa wakipokea fedha kupitia akaunti zao binafsi na kuzitoa kwa matumizi yanayohusishwa na mradi huo kinyume cha taratibu za usimamizi wa fedha za serikali, akisisitiza kuwa tuhuma hizo zinapaswa kuchunguzwa kwa kina na wahusika kuwajibishwa.

Vilevile, amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wa kuwaandikia barua watumishi wanaotuhumiwa badala ya kuchukua hatua za kisheria. 

Sangu amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini hivyo ni wajibu wa viongozi na watumishi kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. 

Ameongeza kuwa atazungumza na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally Chirukie ili kuhakikisha TAKUKURU inakamilisha uchunguzi wake kwa haraka na wale wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo wanafikishwa mahakamani bila kujali nyadhifa zao.

Katika ziara hiyo Mhe. Sangu pia amekagua ujenzi wa shule shikizi ya msingi katika Kijiji cha Kipenzi Kata ya Mfinga ambapo aliahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji na mabati 100 ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo na kuwezesha shule kuanza kupokea wanafunzi mwaka ujao. 

Ziara yake inaendelea katika Jimbo la Kwela ikiwa imelenga kukagua miradi ya maendeleo na kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kuendeleza shughuli za maendeleo jimboni humo.

Post a Comment

0 Comments