Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica E. Yegella, leo Septemba 16, 2026, amefanya matendo ya huruma kwa kutoa msaada kwa Kituo cha Watoto Yatima Nuru, kilichopo Kata ya Ijombe, Kijiji cha Nsongwi Matanji, Wilaya ya Mbeya.
Bi. Yegella amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwapa pole watoto na uongozi wa kituo hicho kufuatia tukio la moto lililosababisha kuungua kwa bweni la watoto wa kike.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Bi. Yegella amesema ameguswa na tukio hilo na kuamua kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
"Nawapa pole kwa kuungua kwa bweni la watoto wa kike. Vitu hivi nilivyoleta vitasaidia katika mahitaji ya watoto,” amesema Bi. Yegella.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Meneja wa Kituo cha Watoto Yatima Nuru, Bi. Mary Himiri amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa moyo wake wa huruma na hatua ya kuwafariji pamoja na kuwasaidia watoto katika kipindi hiki ambacho kituo kinakabiliwa na changamoto hiyo.
Amesema msaada huo ni faraja kubwa kwa watoto na kituo kwa ujumla, huku akieleza kuwa kwa sasa kituo hicho kinahudumia jumla ya watoto 39 wanaolelewa na kutunzwa katika kituo hicho.
Kituo cha Watoto Yatima Nuru kinaendelea na juhudi za kurejesha mazingira bora ya malezi baada ya bweni la watoto wa kike kuungua kwa moto.




0 Comments