Hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuukaribisha mwaka 2026 imetoa dira muhimu kuhusu mustakabali wa amani ya Tanzania, ikisisitiza kuwa utofauti wa kiitikadi haupaswi kuwa sababu ya kulisambaratisha taifa.
Rais ameweka wazi kuwa ingawa ushindani wa mawazo na mitazamo ya kisiasa ni sehemu ya ukomavu wa demokrasia, ni hatari kuruhusu ushindani huo kuvuka mipaka na kugeuka kuwa chuki inayopoteza malengo makuu ya kitaifa.
Onyo hili linakuja wakati nchi bado inatafakari changamoto za amani zilizojitokeza mwezi Oktoba 2025, hatua ambayo Rais ameitumia kupongeza vyombo vya usalama kwa uthabiti wao katika kulinda utulivu wa ndani na kuonesha jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania ina uwezo wa kujiongoza.
Ni lazima jamii itambue kuwa kutumia lugha za kashfa dhidi ya taasisi ya urais hakuleti maendeleo, bali kunazidisha ufa wa utengano ambao maadui wa taifa wanaweza kuutumia kutuvuruga.
Ni wajibu wa kila mwananchi, hususan vijana, kuelewa kuwa nguvu ya taifa haipo katika matusi ya mitandaoni bali katika uwezo wa kujenga nchi kwa vitendo.
Kama sauti za uzalendo zinavyohimiza, nchi yetu ni urithi wa thamani unaohitaji kulindwa kwa busara na si hasira. Matukio ya tarehe 29 Oktoba yanapaswa kuwa kengele ya mwisho ya kutuonya dhidi ya kufuata mikumbo ya chuki. Vijana wasikubali kuwa vibaraka wa kuchochea vurugu ambazo mwisho wa siku zitaharibu kesho yao wenyewe. Madai ya haki ni halali, lakini lazima yatafutwe kupitia ustaarabu na mazungumzo, si kupitia machafuko yanayoweza kutuacha sote tukijuta.
Tunapoingia mwaka 2026, wito wa Rais Samia wa kutaka umoja na mshikamano uwe ajenda kuu unapaswa kuwa mwongozo kwa kila mdau. Viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuwa taa na faraja, wakijitahidi kuunganisha raia na viongozi wao badala ya kuwa sehemu ya kuta zinazotutenganisha.
Tanzania haina mbadala, na kulinda amani yake ni jukumu la kila mmoja wetu, bila kujali vyama tunavyovishabikia au mitazamo yetu ya kidini. Huu ni wakati wa kuponya taifa, kuacha kejeli zisizo na tija, na kusimama pamoja kama Watanzania ili kuifanya nchi yetu iwe mahali pa matumaini na utulivu wa kudumu.

0 Comments