RAIS SAMIA ATOA MKONO WA EID KWA WAZEE ILEMI MBEYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa mkono wa Eid kwa wazee wanaoishi katika Kata ya Ilemi, jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr.

Akiwasililisha zawadi hizo Kwa niaba ya Rais, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia katika kuwajali wazee na makundi maalum, hususan katika nyakati za sikukuu.

“Mheshimiwa Rais amewakumbuka wazee wa Ilemi katika kipindi hiki cha Eid, na ameona ni vyema kuwafikishia mkono wa upendo ili nao waweze kusherehekea kwa furaha kama Watanzania wengine,” amesema Mahundi.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango wa wazee katika jamii na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha ustawi wao unaimarika siku hadi siku.

Baadhi ya wazee waliopokea msaada huo wamemshukuru Rais Samia pamoja na Naibu Waziri Mahundi kwa kuwajali, wakisema msaada huo umewaletea faraja na kuwatia moyo katika kipindi hiki cha sikukuu.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Post a Comment

0 Comments