Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu nchini (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amesema jumuiya hiyo haiungi mkono changamoto au migogoro inayojitokeza nchini, bali inahimiza vijana kushirikiana kutafuta suluhu za changamoto zao kwa hekima na busara.

Kiliba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa serikali za wanafunzi katika Chuo Kikuu Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro, akisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa vijana. 

Amesema ni muhimu kwa vijana kutumia majukwaa ya elimu ya juu kama nafasi ya kuleta suluhu na mawazo yatakayosaidia kuunganisha jamii badala ya kuibua au kuchochea migawanyiko. 

Aidha, amekemea vitendo na kauli zinazolenga kuwagawa Watanzania, akibainisha kuwa matarajio yake ni kuona vyuo vikuu vikichangia kikamilifu katika kutatua changamoto za kijamii na kitaifa kupitia njia za amani na mazungumzo.

Katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro, Rais huyo wa TAHLISO amewataka viongozi wa serikali za wanafunzi nchini kuwa mabalozi wazuri wa amani na uzalendo wa Tanzania, akisisitiza kuwa hakuna changamoto zao ambazo haziwezi kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na amani.

 Kiliba amebainisha hayo wakati akizungumza na Maspika, Mawaziri pamoja na wawakilishi wa serikali za wanafunzi wa jumuiya hiyo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). 

Alifafanua kuwa taarifa mbalimbali zimekuwa zikionesha kuwa baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamekuwa wakiwatumia wanafunzi wa vyuo kama sehemu ya ushiriki wa vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha kutosikilizwa na kutatuliwa kwa kero zao katika vyuo vyao. 

Kiliba amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa kwa kutumia njia za mazungumzo katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili badala ya kukubali kuyumbishwa na makundi ya nje.