Salamu kwa Kijana Mzalendo,
Nakuandikia barua hii nikiwa na imani kubwa na nguvu, akili, na uwezo mkubwa ulionao wa kuibadilisha Tanzania yetu kuwa sehemu bora zaidi. Leo hii, dunia iko kiganjani mwako kupitia simu yako ya mkononi. Mitandao ya kijamii imekupa jukwaa ambalo babu na bibi zetu hawakuwahi kuwa nalo—uwezo wa kusikika na dunia nzima kwa sekunde moja tu. Lakini ndugu yangu, nguvu hii kubwa inakuja na wajibu mkubwa zaidi.
Nimekuwa nikifuatilia mijadala mingi mtandaoni, na inaniumiza kuona jinsi baadhi yetu tunavyotumiwa kama daraja la kuvukisha ajenda za watu wasioitakia mema nchi yetu. Kuna wale ambao "miradi" yao ni kuona Tanzania inawaka moto, watu ambao wanatafuta "bahasha" kupitia vurugu ambazo wewe na mimi ndio tutakaoumia. Wanatuhimiza kususia sherehe zetu za kitaifa, wanatuhimiza kuwatukana viongozi wetu, na wanatupandikiza mbegu ya kukata tamaa kana kwamba hakuna jema linalofanyika.
Ndugu yangu, uzalendo si ushabiki wa chama; uzalendo ni kuipenda ardhi yako na kuheshimu Katiba inayotulinda sote. Tunapomzungumza Rais wetu kwa staha na heshima, hatufanyi hivyo kwa sababu ya "uchawa," bali tunafanya hivyo kwa sababu Rais ni nguzo na alama ya umoja wetu. Ukivunja heshima ya kiongozi wako mbele ya mataifa mengine, unajivunjia heshima wewe mwenyewe na taifa lako.
Ni wakati sasa wa kubadili mwelekeo wa vidole vyetu tunapokuwa kwenye keyboard. Badala ya kutumia saa nane kwa siku kutoa lawama na kashfa ambazo hazileti mkate mezani, kwa nini usitumie muda huo kutafuta fursa? Viongozi kama Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na wengine wapo kwa ajili ya kutengeneza mifumo, lakini ni wewe unayepaswa kuingia uwanjani na kucheza. Tengeneza miradi, andika mawazo yako ya biashara, na utumie mitandao hiyo hiyo kuitangaza.
Kama una changamoto na mtumishi wa umma asiyewajibika, tumia mitandao kutoa taarifa kwa hoja na ushahidi, si kwa matusi. Lugha ya staha ina nguvu ya kubomoa kuta ambazo matusi hayawezi hata kuzitingisha. Kumbuka, kile unachoandika leo ndicho kitakachokusomea miaka kumi ijayo ukiwa unatafuta fursa kubwa za uongozi au biashara kimataifa.
Tukatae kutumiwa. Desemba hii na kuelekea mwaka mpya, tuwaonyeshe wachochezi kuwa "vidonge" vyao vya vurugu havifanyi kazi kwetu. Tuoneshe kuwa sisi ni vijana wa kizazi cha kidijitali kinachojitambua, kizazi kinacholinda amani ya nchi yake kama mboni ya jicho. Amani ndiyo rasilimali pekee tunayoweza kuivuna na kupata faida ya kudumu.
Simama katika uhalisia wako, baki katika uzalendo wako. Tanzania ni yetu sote, na ujenzi wake unahitaji mikono yetu sote, siyo vurugu zetu. Kila jambo litakuwa sawa tukiungana na kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya matumbo ya wachache.
Wako katika ujenzi wa Taifa,
Mtanzania Mzalendo.

0 Comments