Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa taarifa rasmi kuhusu hali ya uzalishaji wa maji, huku ikitangaza kushuka kwa kiasi kikubwa na kuainisha hatua za kiufundi na kiutawala zinazochukuliwa ili kurejesha huduma.
Uzalishaji wa maji umeshuka kutoka lita milioni 534.6 kwa siku hadi lita milioni 270, ikimaanisha upungufu wa lita milioni 264.6 kwa siku, sawa na karibu asilimia 49.5% ya uzalishaji wa awali. Hali hii imeathiri wakazi wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Kama ilivyoelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, hali imekuwa mbaya zaidi katika Mitambo ya Ruvu. Mtambo wa Ruvu Chini, wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 270 kwa siku, kwa sasa unazalisha takribani lita milioni 50 pekee. Aidha, uzalishaji wa Mtambo wa Ruvu Juu nao umeshuka kutoka uwezo wake wa lita milioni 196 hadi kufikia lita milioni 150 kwa siku.
Mhandisi Bwire alibainisha kuwa sababu kuu za upungufu huu ni athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za masika kunyesha chini ya wastani kati ya Machi na Mei, 2025, pamoja na kuchelewa kwa mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba 2025.
Sababu nyingine iliyochangia moja kwa moja ni Mto Ruvu kubadili mkondo wake wa asili katika eneo la Kitomondo na kutengeneza mchepuko.
Katika kukabiliana na changamoto hii, Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu na DAWASA wanatekeleza mikakati ya muda mfupi na mrefu.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmassy, amesema changamoto ya maji iliyotokea inatokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo mengi ya kihuduma.
Kama hatua ya haraka ya kiutawala, Bodi imeendelea na doria ya kukagua vyanzo vyake vya maji katika mito yote na kusitisha utoaji wa vibali kwa watumiaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi hiki cha kiangazi kwa lengo la kuimarisha wingi wa maji. Mhandisi Mmassy alisisitiza kuwa mpaka sasa hali ya mito iko salama na hakuna uchepushaji mwingine wa maji uliopo.
Kwa upande wa mipango ya muda mrefu, miradi mikubwa kama vile Bwawa la Kidunda inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kunakuwepo na hifadhi ya kutosha ya maji na kupunguza utegemezi wa mtiririko wa mto pekee.
DAWASA imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa, kwani utulivu huu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa, ikiwemo upatikanaji wa huduma za msingi.

0 Comments