Katika ulimwengu wa sasa unaokwenda kwa kasi ya mwanga, sheria ambazo haziendani na wakati ni sawa na nanga inayozuia meli ya maendeleo kung'oa nanga.
Hili ndilo lilikuwa chimbuko la safari ya mageuzi ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, alipofanya ziara ya kikazi jijini Dodoma akiambatana na Naibu wake, Mhe. Zainab Katimba. Ziara hii haikuwa ya kiofisi tu, bali ilikuwa ni harakati ya kuhakikisha kuwa mifumo ya kisheria ya Tanzania inabadilika ili kuendana na kasi, maono, na malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwahudumia wananchi.
Dkt. Homera alianza kwa kuweka msisitizo kuwa taasisi zote chini ya wizara yake lazima ziwe na dira inayoeleweka kupitia mipango kazi ya muda mfupi, kati, na muda mrefu.
Akiwa katika Tume ya Kurekebisha Sheria, ukweli mchungu uliwekwa bayana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Winfrida Korosso, aliyebainisha kuwa sheria nyingi nchini zimepitwa na wakati na zimekuwa chanzo cha migogoro isiyo ya lazima katika jamii, hususan miongoni mwa vijana.
Hali hii imemfanya Dkt. Homera kuagiza mapitio ya haraka ya sheria hizo ili ziendane na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi, na kiteknolojia, kukiweka kipaumbele katika utafiti wa kina kabla ya marekebisho kufanyika.
Mapinduzi haya hayakuishia kwenye maandishi pekee, bali yameingia mpaka kwenye utendaji wa kila siku wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Huko, Waziri alijionea jinsi matumizi ya mifumo ya kidijitali yalivyopunguza mrundikano wa majalada na kuharakisha uendeshaji wa mashauri ya jinai.
Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, alithibitisha kuwa teknolojia imekuwa mkombozi katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa weledi uliotukuka. Hatua hii inaungana na jitihada za Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ambayo sasa inatumia mifumo ya TEHAMA kuhakiki sheria ndogo na kuandaa miswada inayozingatia uhalisia wa mabadiliko ya nchi.
Katika upande wa utetezi wa maslahi ya taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga kuhakikisha mikataba yote ya kimataifa inakuwa salama na yenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Naibu Mwanasheria Mkuu, Mh. Samwel Maneno, alisisitiza kuwa wanafanya kazi usiku na mchana kuishauri serikali ili kuzuia mianya ya kisheria inayoweza kugharimu taifa. Hali kadhalika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeelekeza nguvu zake katika kutumia teknolojia kufuatilia uwajibikaji wa taasisi za umma, huku ikizingatia maslahi ya watumishi ili kuleta ufanisi wa kudumu.
Ziara hiyo ilifikia kilele chake Mahakama ya Tanzania, ambapo Dkt. Homera alishuhudia jinsi Mahakama zinazotembea na mifumo ya kisasa ya kupokea malalamiko ilivyopunguza umbali na gharama kwa mwananchi wa kawaida.
Waziri alimalizia kwa kuahidi kuwa Balozi wa taasisi hizo, akizitaka zitoke nje na kujitangaza kwa wananchi ili kila Mtanzania afahamu haki zake na wapi pa kupata huduma. Ni wazi kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Homera, sheria siyo tena kizuizi, bali ni daraja imara linaloiunganisha Tanzania na maendeleo ya kisasa, haki, na utawala bora
0 Comments