Na Gordon Kalulunga
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka mkoa wa Mbeya (NEC) Ndugu Ndele Mwaselela amefanya mambo matatu makubwa kwenye shule ya Sekondari Malama iliyopo Kata ya Nsalala -Mbalizi Mbeya Vijijini.
Mambo hayo matatu ni kutoa Meza 200 na Viti 200, kujitolea gharama za masomo ya jioni kwa wanafunzi wa Kidato cha Pili na Kidato cha Nne na kutoa fedha Taslimu Shilingi Milioni Moja Ili kuanza ujenzi wa matundu ya vyoo vya wavulana shuleni hapo.
Wazazi na wanafunzi walilipuka kwa Shangwe kuu huku yeye akisema kuwa anayafanya hayo yote ikiwa ni ishara ya yale anayowatuma Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dr. Samia Suluhu Hassan.
"Kuanzia sasa wazazi wenye watoto wa Kidato cha Pili na Kidato cha Nne wasichangishwe michango kwa ajili ya walimu masomo ya ziada nitawalipa Mimi chini ya shule yetu ya Paradise Mission Pre and Primary School" Amesema M-NEC Mwaselela huku akishangiliwa na kwamba hiyo ni zawadi kutoka Kwa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan.
Pia amemwelekeza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Aida Haule kuitisha kikao na Madiwani wote Ili kujua changamoto na kuzitatua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Beno Malisa amemshukuru M-NEC Mwaselela akisema kuwa anatimiza kauli mbiu ya Majukumu ya chama ndani ya umma.
Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Mbuba amemshukuru kiongozi huyo na kwamba amegusa Mahitaji sahihi ya umma.
Diwani wa Kata hiyo Festo Mbilike akiwa amejawa na furaha, amesema M-NEC Mwaselela ni chaguo sahihi na kwamba anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kusimamia kikao kilichomteua Mwaselela Kisha kuchaguliwa na wana CCM Mkoa wa Mbeya.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini Ndugu Akimu Mwalupindi ameeleza kwamba M-NEC Mwaselela amekonga nyoyo za wana Mbeya Vijijini kama kiongozi na mdau wa Maendeleo.



0 Comments