Katika mkakati kabambe wa kulinda nguvu kazi ya taifa, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, imeweka bayana kuwa matumizi ya takwimu sahihi na uunganishwaji wa fursa ndiyo njia pekee ya kumfanya kijana wa Kitanzania atulie, aone fursa, na asiyumbishwe na changamoto za sasa na kuwa bendera hufuata upepo.
Hatua hiyo inafuatia maelekezo ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi, Mhe. Joel Nanauka, aliyewataka Maofisa Maendeleo ya Vijana nchi nzima kuwaunganisha vijana na programu za ajira, ujuzi, na uwezeshaji wa kiuchumi.
Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa agizo hili si la kiutendaji tu, bali ni mhimili wa amani na ustawi wa jamii, kwani moja ya sababu kuu zinazowafanya vijana kuyumbishwa na kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa ni hisia za kutelekezwa.
Imeelezwa kuwa maofisa maendeleo wanapokuwa na takwimu sahihi za vijana katika maeneo yao, wanajenga kitu kinachoitwa “Sense of Belonging”.
"Kijana anapotambuliwa mahali alipo na changamoto zake kufahamika, anajihisi kuwa sehemu ya mfumo wa nchi. Hii inajenga uzalendo na kumfanya atulie akijua kuwa serikali inatambua uwepo wake, hali inayopunguza ushawishi wa makundi yanayoweza kuigawa nchi" anasema Nanauka.
Uchunguzi unaonesha kuwa tatizo si ukosefu wa fursa pekee, bali ni "Pengo la Taarifa" (Information Gap) ambazo zinawakabili vijana na hivyo kunatakiwa maofisa hao kuondoa pengo hilo.
" Kuna programu nyingi za kitaifa za ajira na mikopo, lakini kijana wa kijijini au mtaani mara nyingi hajui pa kuanzia." alisisitiza.
Kwa kumfanya Ofisa Maendeleo kuwa "daraja" la moja kwa moja, kijana anaondolewa kwenye hali ya kupapatika. Badala ya kupoteza muda mitaani, kijana sasa anaelekezwa kwenye programu zenye tija, jambo linalomsaidia kuweka malengo ya muda mrefu bila kuyumbishwa.
Pia kutokana na Serikali kubaini kuwepo kwa pengo kati ya mfumo wa elimu na mahitaji ya soko la ajira, maelekezo haya yanalenga kuwapa vijana ujuzi mpya (Reskilling) unaoendana na soko la sasa.
"Kijana mwenye shughuli inayomwingizia kipato cha uhakika hawezi kuyumbishwa na ushawishi wa kisiasa au vitendo vya uvunjifu wa amani," anasema mmoja wa wadau wa maendeleo mkoani Dodoma. Ajira zenye tija ni kinga dhidi ya chuki na machafuko katika jamii yoyote.
Kwa muda mrefu, baadhi ya mifumo imekuwa ikimtazama kijana asiye na ajira kama "tatizo" au "kero". Hata hivyo, Katibu Mkuu, Jenifa Omolo, amesisitiza mabadiliko ya mtazamo. Serikali sasa inamtazama kijana kama fursa inayohitaji kuendelezwa.
Mtazamo huu mpya unaleta matokeo ya haraka kwa sababu mipango sasa inaandaliwa kutokana na uhalisia wa takwimu na hoja za vijana wenyewe (Data-Driven Planning). Hii inaleta matokeo ya kudumu na kurudisha imani ya vijana kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka kipaumbele katika kutatua changamoto za kundi hilo.
Wito wa serikali kwa Maofisa Maendeleo ya Vijana ni wito wa mabadiliko. Ni mkakati unaohakikisha kuwa nguvu, akili, na vipaji vya vijana vinatumika kujenga nchi badala ya kutumika katika mifarakano. Kwa kutumia takwimu na uunganishwaji wa fursa, Tanzania inatengeneza kizazi chenye utulivu, tija, na uzalendo wa dhati.

0 Comments