WADAU MOROGORO WAASA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO, KULINDA UTAMADUNI NA AMANI

Jamii mkoani Morogoro imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili ya Taifa na kudumisha amani, huku wazazi wakionywa kutowaacha watoto wao pekee katika wimbi la ukuaji wa teknolojia ya mitandao ya kijamii.

Akizungumza na wananchi, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Mhe. Sheilla Lukuba, amewataka wazazi kuziba pengo lililopo kati yao na watoto wao katika usimamizi wa matumizi ya mitandao ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

“Nawaomba wazazi tusiache pengo kubwa kwa watoto wetu kwenye suala hili la mitandao. Tumeshaanza kuona madhara yake, hivyo tuendelee kuwasaidia watoto kwa kuwaongoza ili Taifa letu lisitoke kwenye utamaduni ambao babu zetu walituachia,utamaduni wa amani na heshima kwa wakubwa,” alisema Mhe. Lukuba.

Fursa za Kiuchumi kwa Vijana

Kwa upande wake, kijana na fundi ujenzi kutoka Mzumbe, Nuhu Ally, ametoa rai kwa vijana wenzake kuacha kutumia mitandao kama sehemu ya kuchochea vurugu, badala yake waitumie kama daraja la kujikwamua kimaisha.

Alisema mitandao hiyo ikitumika kwa heshima itawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za kibiashara zinazopatikana mtandaoni.

Aidha amewataka vijana wenzake kujiepusha na kuhamasishana mambo yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani nchini.

Kulinda Tunu ya Amani

Naye Mwenyekiti wa Shirika la Kukuza Mila na Desturi Mkoa wa Morogoro (SHIWAMILA), Ramadhan Divunyagale, amesisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kuithamini amani iliyopo na kuliombea Taifa pamoja na viongozi wake.

“Nchi yetu ni nchi ya amani, hivyo Watanzania wote wakiwemo vijana tuendelee kulienzi Taifa letu kwa kudumisha amani na umoja. Tuendelee kumwombea Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ili ituongoze vyema,” alieleza Divunyagale.

Wito huo wa wadau umekuja wakati ambapo mmomonyoko wa maadili na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao yamekuwa yakitajwa kama changamoto inayohitaji nguvu ya pamoja kati ya serikali, viongozi wa kijamii, na wazazi kuanzia ngazi ya familia.

Post a Comment

0 Comments