MARA YAWA KITOVU KIPYA MAGEUZI YA UCHUMI

Mkoa wa Mara umetajwa kuwa kitovu kipya cha mageuzi ya kiuchumi nchini kufuatia mwitikio mkubwa wa wawekezaji wa ndani waliojitokeza kuchangamkia fursa mbalimbali, hatua inayotajwa kuwa nguzo muhimu katika kulinda utulivu wa nchi na kutengeneza ajira kwa vijana.

Katika Kongamano la Uwekezaji wa Ndani lililofanyika Januari 26, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wadau wa maendeleo na wafanyabiashara kutoka Kanda ya Ziwa wamehimizwa kuwekeza kwa uzalendo ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Balozi Dkt. Aziz Mlima, amebainisha kuwa uwekezaji wa wazawa ni ishara ya uzalendo uliotukuka.

"Wawekezaji wa ndani wanapomiliki uchumi wao, wanajenga msingi imara wa amani na utulivu wa nchi. Tunapokuwa na uchumi jumuishi unaoshirikisha Watanzania wenyewe, tunapunguza utegemezi na kuimarisha usalama wa Taifa letu," alisema Dkt. Mlima.

Kongamano hilo limeibua matumaini mapya kwa maelfu ya vijana mkoani Mara na Kanda ya Ziwa. Kupitia miradi itakayosajiliwa chini ya TISEZA, fursa za ajira za kudumu na za muda zinatarajiwa kuongezeka, hali itakayopunguza wimbi la ukosefu wa ajira na kuongeza tija katika nguvu kazi ya Taifa.

Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani (TISEZA), Bw. Felix Michael, aliwasilisha mwongozo wa sekta za kipaumbele zinazohitaji uwekezaji wa haraka ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kisasa na shindani ifikapo mwaka 2050.

Aidha kuna faida kubwa zitolewazo na Serikali kupitia TISEZA  ili kufanikisha uwekezaji huo ikiwamo,punguzo la kodi kwa mitambo na malighafi za uzalishaji; urahisi wa kupata ardhi na vibali vya biashara na kuwepo kwa miundombinu ya kisasa katika maeneo maalumu ya uwekezaji (EPZ/SEZ).

Mwitikio huu wa mkoani Mara unadhihirisha kuwa kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani inazaa matunda. Kwa kuimarisha sekta binafsi ya ndani, Tanzania inajipanga vyema kutekeleza Dira 2050 kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wake kwa njia endelevu.

Post a Comment

0 Comments