VETA INAPOWAJENGEA VIJANA "JICHO LA BIASHARA"


Katika ulimwengu wa sasa wa ushindani wa kibiashara, kumpa kijana ujuzi wa kutengeneza samani au kushona nguo bila kumfundisha jinsi ya kuishawishi jamii kununua bidhaa hiyo, ni sawa na kumpa silaha askari asiye na mafunzo ya shabaha. Huu ndio ukweli mchungu uliotawala ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha VETA Chemba, mkoani Dodoma, Januari 24, 2026.

Ushauri wa kamati hiyo kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) haukuwa wa kawaida; ulikuwa ni wito wa mabadiliko ya mtaala (Curriculum shift) kutoka kwenye "Ufundi wa Mazoea" kwenda kwenye "Ufundi wa Kibiashara."

Wabunge Yumna Mmanga Omar na Asha Baraka wamegusa donda ndugu la vijana wengi wa kitanzania wanaohitimu mafunzo ya ufundi. Wengi wao wana uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zenye ubora, lakini wanakosa uwezo wa kupanga Bei (Pricing Strategy) kwa kujua gharama ya uzalishaji dhidi ya faida.

Pamoja na ukweli kuwa bidhaa nyingi za VETA ni bora,  muonekano wake hauashirii thamani hiyo  na hivyo ipo haja ya kuhakikisha kuwa vijana hao wanajua namna ya kuiweka bidhaa yao katika thamani halisi.

Pia wabunge hao wameelezea haja ya kusisistiza matumizi ya teknolojia ya masoko kwa kutumia mifumo ya kidijitali kupata wateja nje ya eneo lao la kijiografia.

"Kujiajiri siyo kuwa na karakana tu; ni kuwa na wateja. Kijana anaweza kuwa fundi mzuri wa umeme, lakini kama hajui jinsi ya kujiuza (Self-branding) ili apate tenda  (zabuni), atabaki mtaani akilalamika hana ajira wakati ujuzi anao mkononi," walisisitiza wabunge hao.

Mwenyekiti wa Kamati, Husna Sekiboko, amesisitiza jambo lingine la kiufundi la ubunifu kulingana na mahitaji ya wakati. VETA imetakiwa kuacha kufundisha wanafunzi kutengeneza bidhaa za kizamani ambazo soko halizitaki tena.

Leo hii jamii inahitaji bidhaa zinazookoa nishati, vifaa vya kidijitali, na mavazi ya kisasa. Ikiwa VETA itawajengea uwezo wa kufanya utafiti wa soko (Market Research), mwanafunzi hatazalisha bidhaa kwa sababu "anajua kuitengeneza," bali atazalisha kwa sababu "soko linaihitaji." Hii ndiyo tofauti kati ya fundi na mjasiriamali.

Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanashauri kuwa VETA sasa inapaswa kuingiza somo la "Stadi za Masoko na Mauzo" (Marketing and Sales Skills) kama somo la lazima kwa kila kozi. Hii itamfanya fundi kompyuta wa VETA asijue tu kutengeneza bodi (Motherboards), bali ajue pia jinsi ya kuandika andiko la biashara (Business Proposal) la kutoa huduma za matengenezo kwenye ofisi kubwa.

Ikiwa VETA itafanikiwa kuunganisha ujuzi wa mikono na ujuzi wa masoko, tutashuhudia kundi kubwa la vijana likiacha kusubiri ajira serikalini na badala yake kuanza kuajiri wengine. Hii ndiyo njia pekee ya kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Post a Comment

0 Comments