NAIBU WAZIRI MAHUNDI ASISITIZA UWAJIBIKAJI MIRADI VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII.

📌 Aagiza Bweni la Wasichana Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole likamilishwe kwa wakati.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa bweni la wasichana katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole, Jijini Mbeya, kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuendana na malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa kike.

Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa maagizo hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni hayo, ambayo yamefikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji wake huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo.

“Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni tano katika ujenzi wa bweni hili, hivyo ni wajibu wa mkandarasi, msimamizi wa mradi na uongozi wa Chuo kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na mradi huu unakamilika kwa ubora na kwa wakati,” amesema Mhe. Mahundi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mbeya Edina Mwaigomole amesema ujenzi wa bweni hilo ni hatua muhimu katika kumlinda na kumwezesha mtoto wa kike kielimu, hasa kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.

“Bweni hili ni suluhisho la changamoto nyingi zilizokuwa zinawakabili wasichana, ikiwemo ukosefu wa makazi salama. UWT tunaipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowasaidia wasichana kusoma kwa utulivu na kujiendeleza,” amesema Mwenyekiti Edina.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole, Silvester Mwambene, amesema kukamilika kwa mabweni hayo kutakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike pamoja na kupunguza changamoto za kijamii zilizokuwa zikijitokeza awali.

“Mabweni haya yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 600 na yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike, kwani yatatoa mazingira salama na rafiki kwa masomo,” amesema Mwambene.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa mabweni hayo, Latoi Mollel, amesema maandalizi ya mwisho yanaendelea na mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.

Post a Comment

0 Comments