Uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme vijijini umetajwa kuwa mkakati madhubuti wa kuleta amani ya kudumu na haki ya kiuchumi kwa vijana, huku ukiwakumbusha wajibu wao wa kulinda mali za umma.
Katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amebainisha kuwa uwekezaji wa serikali wa shilingi bilioni 323 katika mradi wa umemejua wilayani Kishapu, ni hatua ya makusudi ya kuhakikisha vijana wanapata haki yao ya msingi ya kushiriki katika uchumi wa kisasa.
Mradi huu wa kimkakati ni kielelezo cha namna nishati inavyoweza kugeuza fikra za vijana kutoka kwenye mipango isiyo na tija kuelekea kwenye uwajibikaji, kwani tayari umetoa ajira 560 ambapo vijana 67 ni wakazi wa maeneo ya mradi.
Kwa kupeleka umeme vijijini serikali inatengeneza mazingira ambapo kijana anawajibika kwa kazi na kuacha kufikiria vitendo vya uvunjifu wa amani au upuuzi unaoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Uwepo wa nishati hii ni kielelezo cha haki kwa vijana wa vijijini ambao sasa wanaweza kufurahia fursa sawa na wale wa mijini, jambo linalopunguza malalamiko na migawanyiko katika jamii.
Kupitia umeme wa uhakika, vijana wanajengewa mwelekeo chanya wa kimaisha ambapo badala ya kutumiwa na wanasiasa wakora au kuchochea fujo, wanatumia akili zao kubuni teknolojia na kuongeza thamani ya mazao kama asali na kilimo.
Hali hii inathibitisha kuwa amani ya kweli inapatikana pale kijana anapokuwa na kazi ya kufanya, kwani akili isiyo na kazi ni karakana ya shetani, na nishati ya umeme inakuja kama suluhu ya kumpatia kijana mnyororo wa thamani utakaomfanya athamini utulivu wa nchi yake kwa ajili ya kulinda biashara yake.
Pamoja na haki hiyo ya kupata nishati, Mhe. Makamba amesisitiza wajibu wa vijana kama walinzi wa kwanza wa miundombinu ya taifa. Onyo kali limetolewa dhidi ya vitendo vya wizi wa vifaa vya mradi huo wa umemejua, kwani kuhujumu mali hizi ni kujinyima haki ya maendeleo na kuvuruga amani ya kiuchumi.
Kila kijana anapaswa kutambua kuwa wajibu wake ni kulinda kila nguzo na kila kifaa cha mradi huo hadi kukamilika kwake Januari 30, 2026, kwani kufanya hivyo ni kulinda mustakabali wa maisha yake. Serikali inapowekeza mabilioni ya fedha, inafanya hivyo kwa imani kuwa vijana wataonyesha uzalendo kwa kutunza mazingira na miundombinu hiyo ili iwaletee tija ya muda mrefu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, ameongeza kuwa kupatikana kwa umeme katika vitongoji kama Majengo na Kata ya Wendele ni chachu ya mshikamano wa kitaifa kupitia kazi. Haki ya kijana kupata nishati inamfanya ajihisi sehemu ya taifa, na wajibu wake wa kuzalisha mali unamfanya awe mwananchi anayeheshimu sheria na amani.
Kwa kutumia umeme katika shughuli za kikarakana na usindikaji, vijana wanakuwa na sauti moja katika kudai maendeleo badala ya vurugu, hali inayofanya Tanzania iendelee kuwa kitovu cha utulivu. Hivyo, mradi wa umemejua Kishapu si tu mradi wa nishati, bali ni mradi wa amani unaowafundisha vijana kuwa haki yao ya kiuchumi inaendana sambamba na wajibu wao wa kulinda na kuheshimu amani ya nchi.

0 Comments