ULEVI WA POMBE KWA VIJANA NI CHANGAMOTO MPYA BAADA YA DAWA ZA KULEVYA KUDHIBITIWA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeeleza kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini, changamoto mpya ya ulevi wa pombe imeibuka, hasa miongoni mwa vijana.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha mamlaka hiyo na Wahariri pamoja na waandishi wa habari, chenye lengo la kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Lyimo aliongeza kuwa ulevi wa pombe kupindukia una athari kubwa kwa jamii ikiwemo kupoteza nguvu kazi, uraibu, na kudhorota kwa afya za wat watumiaji kupoteza tija ya vijana, hivyo ni muhimu waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu na kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya pombe.

  "Matumizi ya pombe yanafaakutumiwa kwa kiasi ili kuendelea kuwa na vijana na taifa lenye jamii imara".

Amesema kwa sasa Tanzania imefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa biashara ya dawa za kulevya kutokana na mchango wa waandishi wa habari katika kutoa elimu kwa jamii na kuonesha uhalisia wa athari za dawa hizo.

 “Kupitia ninyi waandishi wa habari tumeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa. Mmefanikiwa kutoa elimu kwa jamii kwa kuonesha madhara na uhalisia wa dawa za kulevya,” amesema Lyimo.

Ameeleza kuwa bila vyombo vya habari, DCEA isingeweza kufikia malengo yake kikamilifu kwani mamlaka hiyo ina kitengo cha uelimishaji kinachofikia makundi mbalimbali, lakini vyombo vya habari vina uwezo wa kuwafikia wananchi wengi kwa muda mfupi zaidi.

 “Sisi kama DCEA hatuwezi kuwafikia Watanzania wote kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya, lakini vyombo vya habari vinafanya kazi hiyo kwa haraka na kwa wigo mpana zaidi,” ameongeza.

Kamishna Jenerali huyo amesisitiza kuwa tatizo la dawa za kulevya ni janga la kimataifa linalovuka mipaka ya nchi, na athari zake hugusa nyanja zote za maisha ikiwa ni pamoja na kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiafya na kimaendeleo.

  “Ukitaka kuua taifa lolote kijamii, kisiasa, kiuchumi na kifikra, peleka dawa za kulevya. Taifa haliwezi kuendelea,” amesema.

Aidha, amesema dawa za kulevya ni mlango wa kuingia katika masuala ya ugaidi, akibainisha kuwa magaidi wengi hutumia dawa hizo ili kupata ujasiri wa kutekeleza vitendo vya utekaji, mauaji na kujitoa muhanga.

 “Tunapodhibiti dawa za kulevya, tunadhibiti pia masuala ya ugaidi,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio hayo, changamoto mpya ya ulevi wa pombe, hasa miongoni mwa vijana, imeibuka na inahitaji nguvu ya pamoja kuikabili.

  “Sasa hivi ukienda kwenye sober house, zamani wengi walikuwa waraibu wa dawa za kulevya, lakini sasa wengi ni waraibu wa pombe. Tunaomba vyombo vya habari mtusaidie kutoa elimu ya kujiepusha na ulevi uliopindukia,” amesema.

Amefafanua kuwa pombe inapaswa kutumiwa kwa kiasi, lakini kwa dawa za kulevya hakuna kiwango chochote kinachoruhusiwa kwani ni marufuku kabisa.

Kamishna Lyimo ameahidi kuwa DCEA itaendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya namna bora ya kuripoti masuala ya dawa za kulevya, huku akieleza kuwa biashara hiyo mara nyingi huambatana na rushwa, hali iliyosababisha mamlaka hiyo kushirikiana na TAKUKURU kuwabaini wahusika.

 “Uhalifu wa dawa za kulevya ni wa kupangwa na unavuka mipaka,” amesema.

Pia amewahimiza wananchi kutoa taarifa zozote zinazohusiana na dawa za kulevya kupitia namba 119, akibainisha kuwa mtu yeyote atakayetoa taarifa itakayosaidia kukamatwa kwa dawa au kuvunja mtandao wake atapata zawadi nono

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, amesema waandishi wa habari wana nafasi ya kufanya uandishi wa kuvuka mipaka kwa kushirikiana na waandishi wa nchi jirani au nchi yoyote duniani katika kufichua mitandao ya dawa za kulevya.

Amesisitiza pia umuhimu wa vyombo vya habari kushirikishwa wakati wa operesheni za kukamata au kuteketeza dawa za kulevya ili kuripoti matukio hayo kwa kuzingatia weledi wa uandishi wa habari.

Naye John Bukuku, mmoja wa wachokoza mada, ameiomba DCEA kuendelea kuboresha mbinu za mawasiliano kwa kutumia mitandao ya kijamii hususan blogu, akisema ndiyo hazina kuu ya taarifa duniani kwa sasa

Washiriki wengine akiwemo Hussein Manane, Elizabeth kutoka Nipashe na Jerome Risasi wa Clouds Media wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa waandishi wa habari, kuwawezesha kifedha na kitaaluma ili waweze kutengeneza vipindi na taarifa zenye athari chanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini

Post a Comment

0 Comments