Serikali imetangaza kutoa kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuwawezesha watengeneza maudhui ya kidijitali (Content Creators) nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya habari, sanaa na michezo.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema fedha hizo zinalenga kuwasaidia wabunifu hao kuimarisha kazi zao, kununua vifaa vya kisasa na kuongeza kipato kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
Nyanja zitakazonufaika Waziri Makonda amebainisha kuwa fursa hiyo haitakuwa na upendeleo, bali itagusa makundi yote yanayojishughulisha na uzalishaji wa maudhui katika sekta za: Utalii na michezo;Habari na burudani;Muziki, filamu na sanaa za maonesho na Maudhui ya kijamii na elimu.
Utaratibu wa Maombi
Aidha, Mhe. Makonda amewataka vijana wote wanaojihusisha na kazi hizo kutochezea fursa hiyo adhimu, akitangaza kuwa zoezi la uandikishaji limeanza rasmi leo Januari 30 na litahitimishwa Februari 15, 2026.
"Watengenezaji wa maudhui wanatakiwa kufika katika ofisi za halmashauri za wilaya, manispaa za miji na majiji kupitia vitengo vya habari ili kuchukua na kujaza fomu za maombi, zikiainisha taarifa binafsi pamoja na shughuli wanazozifanya," alisema Waziri Makonda.
Mapokezi ya Wadau
Hatua hiyo imepokelewa kwa kishindo na wadau wa kazi za kidijitali, ambao wameipongeza Serikali kwa kutambua rasmi mchango wa "Content Creation" kama sekta rasmi ya ajira inayoweza kuliingizia taifa mapato na kuitangaza nchi kimataifa.
Baadhi ya vijana waliohojiwa wamesema hatua hiyo itawapa morali na nidhamu ya kazi, huku wakiahidi kutumia fedha hizo kuleta mapinduzi ya kiteknolojia katika kazi zao ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa.

0 Comments