MATUNDA ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha elimu ya ufundi na vyuo vya kati yameanza kuonekana dhahiri, baada ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Mbeya kuzindua mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu uliotengenezwa na wataalamu wa ndani.
Mtambo huo, ambao ni wa kwanza wa aina yake mkoani hapa, umetajwa kuwa ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wa kati kwani utaondoa matumizi ya zebaki—kemikali hatarishi kwa afya na mazingira ambayo imekuwa ikitumiwa kwa miaka mingi kutokana na ukosefu wa teknolojia mbadala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, uongozi wa SIDO Mbeya umebainisha kuwa mtambo huo ni matokeo ya maboresho makubwa yaliyofanywa katika karakana za Kituo cha Uendelezaji wa Teknolojia (TDC). Wataalamu waliohitimu katika vyuo vya ufundi na kati nchini wametumia ujuzi wao kubuni mashine hiyo kulingana na mahitaji halisi ya wachimbaji wa Kitanzania.
"Lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi. Mtambo huu utawasaidia wachimbaji kusafisha dhahabu kwa haraka, usalama na kwa tija zaidi, tofauti na mbinu duni za zamani," ilieleza taarifa ya SIDO.
Mageuzi ya Mashirika ya Umma
Uvumbuzi huu wa SIDO unaendana na mkakati mpana wa Serikali wa kufanya mageuzi makubwa ndani ya Mashirika ya Umma kuelekea mwaka 2030. Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi na uwazi ili mashirika haya yachangie angalau asilimia 10 ya mapato yote yasiyo ya kodi.
Taarifa rasmi za Serikali zinaonyesha kuwa nia ni kuyajengea uwezo mashirika kama SIDO, STAMICO na mengineyo yaweze kushindana kimataifa na hata kuwekeza nje ya mipaka ya Tanzania, kama yanavyofanya mashirika ya kigeni yaliyopo nchini.
Uwajibikaji na Huduma kwa Wananchi
Mbali na mapinduzi ya viwanda, Serikali imesisitiza kuendelea kupambana na rushwa, ubadhirifu na uzembe maofisini ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi. Hatua za kuimarisha nidhamu na mifumo ya upimaji wa utendaji kazi (OPRAS) zimeendelea kuchukuliwa ili kuleta matokeo ya vitendo kama haya yanayoonekana SIDO Mbeya.
Kwa upande wao, baadhi ya wachimbaji wadogo mkoani Mbeya wameipongeza hatua hiyo wakisema kuwa teknolojia hiyo itapunguza gharama za uchenjuaji na kulinda afya zao, jambo ambalo ni kielelezo cha uongozi unaojali utu na maendeleo ya watu wa hali ya chini.

0 Comments