WAKATI Taifa likisonga mbele, sauti za Watanzania kutoka makundi mbalimbali zimeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu, huku onyo kali likitolewa kwa vijana dhidi ya kutumia mitandao ya kijamii kama sehemu ya kuchochea chuki, matusi na vurugu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi na wadau wa maendeleo wamebainisha kuwa matumizi ya mitandao hayana faida yoyote ikiwa yatatumika kuchafua amani ya nchi, na badala yake imehimizwa kutumika kama nyenzo ya ujenzi wa Taifa.
Katika ujumbe mzito uliosambaa kwa vijana nchini, imesisitizwa kuwa mwaka 2026 haukuja kwa ajili ya kelele, jazba au ushabiki wa upofu, bali umebeba ujumbe wa busara, uwajibikaji na kazi. Vijana wameaswa kuelewa kuwa haki haitafutwi kwa kuchoma nchi wala kupandikiza chuki kwa misingi ya siasa, dini au makabila.
"Haki hupatikana kwa kutumia akili, sheria na njia halali. Yaliyotokea mwaka 2025 yawe funzo na sio silaha ya kulipiza visasi. Taifa letu linahitaji uponyaji na mshikamano," ulieleza ujumbe huo uliowataka vijana kuacha kuwa zana za wachochezi.
Kwa upande wao, wakazi wa Dar es Salaam wameelezea kuwa amani haina mbadala na ndiyo msingi wa shughuli zote za kiuchumi. Saidi Gulu, mkazi na mjasiriamali wa Temeke, alisisitiza kuwa bila amani hakuna maendeleo.
"Ili tuendelee na shughuli zetu za kila siku, sharti amani na utulivu viwepo. Lazima tuzidi kushikamana na kufanya maendeleo kwa ajili ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla," alisema Gulu.
Naye Pius Philemon, mkazi wa Sandali na Ofisa Usafirishaji, alibainisha kuwa amani ni mtaji namba moja kwa wafanyabiashara. "Bila amani hatuwezi kufanya shughuli zetu na hatuko tayari kuona watu wanaharibu amani iliyopo. Tunahitaji mshikamano wa kudumu ili tujiletee maendeleo."
Wito umetolewa kwa vijana kutumia ujuzi wao kama mtaji na nidhamu kama chapa yao kuu. Obadia William, mkazi wa Tabata Kimanga, amewasihi Watanzania kuachana na ushawishi mbaya na badala yake kudumisha mshikamano waliojengewa na viongozi wao.
"Mambo ya vurugu hatujayazoea. Tunahitaji utulivu ili tufanye shughuli zetu. Amani na utulivu havina mbadala, tuhakikishe tunavilinda kwa maendeleo ya nchi yetu," alisema William.
Habari hii inahitimishwa kwa kuwakumbusha vijana kuwa mustakabali wa Tanzania uko mikononi mwao. Taifa halijengwi kwa hasira au propaganda, bali kwa jasho, ubunifu na uvumilivu. Vijana wametakiwa kusimama kama watu wenye fikra huru wanaojali kesho ya nchi yao kwa kutumia mitandao kujenga na kuunganisha, badala ya kubomoa na kugawanya.

0 Comments