MAONO YA RAIS SAMIA YALETA MAPINDUZI MAKUBWA HIFADHI YA JAMII

TANZANIA imetandika rekodi mpya ya kihistoria katika sekta ya Kinga ya Jamii ikiwa ni miongoni mwa nchi 17 zenye mifumo bora zaidi ya hifadhi ya jamii. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni kielelezo cha mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha ustawi wa wananchi wake.

Akihitimisha mkutano wa siku mbili wa wadau wa sekta ya Kinga ya Jamii jijini Arusha, Februari 10, 2026, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewataka watendaji wote nchini kuyaishi maono ya Mheshimiwa Rais kwa vitendo ili kuhakikisha malengo ya kitaifa yanayokusudiwa yanafikiwa kikamilifu.

Alisema mafanikio yaliyofikiwa sasa, hayakuja kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuinua hali ya maisha na kutoa kinga ya uhakika kwa kila mwananchi nchini.

Aliwataka wote wanaohusika na utekelezaji wa sera ya kinga ya jamii kuhakikisha kwamba wanatekeleza wajibu wao kwa tija kubwa ili kuleta nafuyu kwa wananchi wa kawaida hasa ikizingatiwa kwamba sera hiyo inazinduliwa huku kukiwa na mafanikio makubwa kwenye taasisi zinazosimamia hifadhi ya jamii.

Sekta ya hifadhi ya jamii nchini imeshuhudia ukuaji wa kishindo ambao haujawahi kutokea ndani ya kipindi kifupi. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, ameanika takwimu zinazonesha namna thamani ya mifuko ya hifadhi ilivyopaa kutoka Shilingi trilioni 10.43 mwaka 2020 hadi kufikia Shilingi trilioni 24.20 mwezi Desemba 2025.

Ongezeko hilo la thamani ya mifuko ambalo ni zaidi ya asilimia 130, limeenda sambamba na kuimarika kwa Mfuko wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) ambao umefanikiwa kugusa maisha ya watu milioni 5.5 kupitia ruzuku ya Shilingi trilioni 1.55. Hatua hii inathibitisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutoacha mtu yeyote nyuma katika safari ya maendeleo.

Moja ya habari kubwa iliyoibuka kwenye mkutano huo ni kuzinduliwa kwa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 pamoja na Skimu ya Hifadhi kwa Waliojiajiri.

 Hatua hii imetajwa kuwa ni mkombozi kwa mamilioni ya Watanzania wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi, wakiwemo mama lishe, waendesha bodaboda na wafanyabiashara wadogo, ambao sasa wanaweza kuwa na akiba na kinga ya uhakika kwa maisha yao ya baadaye.

Tanzania sasa inatekeleza misingi yote tisa ya hifadhi ya jamii, ikiwemo Fao la Familia ambalo linahakikisha upatikanaji wa elimu bure, matibabu kwa wazee, watoto na akina mama kupitia mchango wa Serikali. "Ndoto ya Watanzania kuwa ndani ya mfumo wa hifadhi ya jamii sasa inakwenda kukamilika," alisisitiza Mhe. Ridhiwani Kikwete.

Mkutano huo uliowakutanisha wadau takribani 1,000 umeibua maazimio manne ya kimkakati ambayo yatafanyiwa kazi na Ofisi ya Waziri Mkuu. Maazimio hayo ni pamoja na kuhimiza Mfuko wa WCF kuingiza waliojiajiri kwenye mifumo ya fidia, na kupendekeza elimu ya kinga ya jamii ianze kufundishwa kuanzia ngazi ya Vyuo Vikuu ili kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa vijana.

Aidha, wadau wamehimiza usimamizi madhubuti wa sheria ambapo waajiri wanatakiwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, pamoja na kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa umma ili kuondoa upotoshaji kuhusu mifumo ya hifadhi. 

Katibu Mkuu, Mary Maganga, amewahakikishia washiriki kuwa ofisi yake imejipanga kufanyia kazi maoni hayo kwa weledi ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kijamii na kiuchumi nchini.

Post a Comment

0 Comments