WAZIRI SANGU: MAHUSIANO, AMANI NA UMOJA NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amesema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuanzisha Wizara maalum yenye dhamana ya kushughulikia masuala ya Mahusiano inaakisi maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha Umoja, Mshikamano na Amani nchini.

“Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye amani, mshikamano na maendeleo kupitia mazungumzo, maridhiano na ushirikiano wa wadau wote,” amesema

Mhe. Sangu amesema hayo Juni 28, 2026 katika Ibada maalumu ya kilele cha harambee iliyofanyika kwenye ushirika wa Amani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, mjini Singida ambapo alieleza kuwa Serikali imeendelea kujenga mazingira ya mazungumzo na ushirikiano kati yake na taasisi za dini ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu Mahusiano ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kutimiza wito wa kibiblia wa kuwaleta watu pamoja bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.

Vile vile, Waziri Sangu amempongeza Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kusimamia karibu agenda ya mahusiano nchini, jambo ambalo limewezesha viongozi wa dini kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao serikalini kupitia wizara hiyo, hatua ambayo imeongeza ushirikiano na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Aidha, alisema jukumu la kuwasikiliza wananchi, hususan wanyonge na wenye mahitaji, ni sehemu ya wajibu wa Serikali na linaendana na mafundisho ya dini yanayohimiza kuwajali wahitaji na kujenga jamii yenye haki na mshikamano.

Kwa upande mwengine, Waziri Sangu aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake, na kusema maombi yao yamekuwa nguzo muhimu katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya nchini.

Kadhalika, Mhe. Sangu amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini pamoja na wadau wengine katika kuimarisha mahusiano ya kijamii na kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya mazungumzo na vyama vya siasa kwa lengo la kuimarisha umoja wa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments