PROF. KABUDI AFUNGUKA MAZITO: UPELELEZI, MARIDHIANO NA KATIBA MPYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ametoa ufafanuzi mzito kupitia mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), akibainisha hatua zinazofuata baada ya ripoti ya tume kubaini kuwepo kwa vikundi vilivyopanga na kufadhili ghasia za uchaguzi. 

Profesa Kabudi ameweka wazi kuwa kazi iliyofanyika na Tume ya Jaji Chande ilikuwa ni kutafuta ukweli na ukusanyaji wa taarifa ambapo imebainika wazi kuwa kuna kundi lililojipanga, likafadhili, na hata kukusanya vijana kwenye makambi kwa ajili ya mafunzo ya uhalifu, na kusisitiza kuwa watu hao hawawezi kuwa sehemu ya serikali bali ni kundi linalofahamika.

Akifafanua kuhusu hatua za kisheria, Profesa Kabudi amesema kuwa baada ya kukamilika kwa kazi hiyo ya kutafuta ukweli, sasa hatua inayofuata ni upelelezi wa kina ambapo wale wote waliohusika lazima wapewe haki yao ya kuitwa mbele ya vyombo vya upelelezi ili kujibu tuhuma zinazowakabili. 

Amesema kuwa hiyo ndiyo kazi ya msingi ya upelelezi na hakuna mhusika atakayekwepa mkono wa sheria kwani utambulisho wao uko wazi na ni lazima hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria za nchi.

Waziri huyo amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, nchi itakuwa ikitekeleza mambo matatu makubwa kwa mpigo ambayo ni upelelezi kwa waliofanya makosa, mchakato wa maridhiano, na maandalizi ya Katiba Mpya. 

Amefafanua kuwa Tume ya Maridhiano itaundwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ili kuhakikisha ushirikishi wa kila mwananchi, huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina utashi mkubwa wa kisiasa wa kuhakikisha mchakato huo unafanikiwa na kuleta utulivu wa kudumu.

Kuhusu suala la Katiba Mpya, Profesa Kabudi ametoa matumaini makubwa kwa Watanzania akisema kuwa mahali pa kuanzia tayari papo na utashi wa Rais ni kielelezo tosha kuwa Katiba itapatikana. Amesisitiza kuwa tume imependekeza Katiba hiyo mpya ipatikane ifikapo mwaka 2028, na akaongeza kuwa ikiwa wale wenye nia mbaya wataacha kuweka vitimbi na kuzuia mchakato huo, Watanzania watapata Katiba yenye matakwa yao na inayozingatia maslahi ya taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments