RAIS SAMIA AZINDUA MELI YA KWANZA YA UVUVI WA BAHARI KUU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), akisema hatua hiyo ni msingi muhimu katika kuimarisha mchango wa sekta ya uvuvi kwenye uchumi wa taifa.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumamosi Aprili 25, 2026, katika hafla iliyofanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Samia ameeleza kuwa uwekezaji huo unaakisi dhamira ya serikali katika kutekeleza sera na mikakati ya kukuza uchumi wa buluu.

Amesema meli hiyo si chombo cha kuvulia samaki pekee, bali ni sehemu ya mfumo mpana unaounganisha uzalishaji wa ndani, uvuvi wa kisasa pamoja na masoko, hatua itakayosaidia kuongeza tija na thamani ya rasilimali za bahari kuu.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa serikali imejipanga kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili liweze kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za bahari kuu na kuhakikisha manufaa yake yanawanufaisha Watanzania.

Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti uvuvi haramu, usiozingatia sheria, akisema serikali itaendelea kuimarisha mamlaka zake ili kulinda mazingira ya bahari na viumbe wa majini.

Pia ameieleza kuwa jitihada zimefanyika kuboresha mazingira ya uvuvi katika maziwa kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji, utaalamu na vifaa, ikiwemo boti za uvuvi pamoja na mbinu za kisasa za ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.

Rais Samia ameongeza kuwa serikali inaendelea na mchakato wa kununua meli nyingine nne za uvuvi pamoja na meli ya mafunzo na utafiti, ili kuongeza uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu na kuongeza ushindani wa kiuchumi.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo na kuunga mkono mikakati ya serikali, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Post a Comment

0 Comments