TANZANIA YAPATA USHINDI MKUBWA UNESCO: Wazushi Waaibika, Dunia Yazidi Kuiamini

Jaribio la wazushi na wapachika uongo wa mitandaoni la kutaka kuitenga Tanzania na jumuiya ya kimataifa limeambulia patupu baada ya ulimwengu kudhihirisha imani kubwa kwa Tanzania , kufuatia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kundi la Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka miwili, sambamba na kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).


Uchaguzi huo, uliotangazwa katika Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea mjini Busan, Jamhuri ya Korea, ni ushahidi tosha kuwa harakati za upotoshaji mtandaoni zimeshindwa kabisa kuificha Tanzania duniani, kwani badala ya kutengwa, dunia imezidi kuiamini Tanzania na kuikabidhi majukumu makubwa zaidi ya uongozi na uratibu wa masuala ya kimataifa, ikiwemo kuratibu misimamo ya Kundi la Afrika, kuongoza majadiliano ya bara, na kuhakikisha maslahi ya urithi wa dunia yanalindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Hatua hiyo si tu heshima kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uthibitisho wa nafasi yake inayozidi kuimarika katika diplomasia ya kimataifa, bali pia ni pigo kubwa kwa wale wote wanaojaribu kupotosha ukweli kwa maslahi binafsi ya kisiasa na kimtandao. Hali hii inaonyesha kuwa sifa ya Tanzania kama nchi inayojenga maridhiano, inayozingatia amani, na yenye ushiriki wenye tija ndani ya UNESCO inasalia imara isiyotikisika.


Ushindi huu ni wa wananchi wote wa Tanzania wanaoamini katika amani, utulivu, na kupiga hatua katika maendeleo. Wakati wazushi wakiendelea na upotoshaji wao wa bure mitandaoni, viongozi na wawakilishi wa nchi wanazidi kusonga mbele; ambapo katika mkutano huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, alitumia jukwaa hilo kuzungumza na Kamati ya Ushauri ya masuala ya Uhifadhi wa Maeneo ya Urithi wa Asili ya UNESCO na kushiriki vikao vya kimkakati kueleza hatua kubwa zinazochukuliwa na Tanzania kulinda maeneo ya urithi kama Ngorongoro na Serengeti.


Huu ni ushahidi thabiti kuwa uongozi wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa unabaki kuwa nguzo ya kuaminika, na jitihada zote za wazushi wa mitandaoni zimegonga mwamba mbele ya mafanikio ya kishindo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments