Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa zinazohusu vitendo vya uvunjifu wa sheria za mipaka, viashiria vya uhalifu, na matukio mengine yanayoweza kuhatarisha usalama, kwa lengo la kulinda usalama wa taifa na maslahi mapana ya nchi.
Ametoa wito huo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi ya Uhamiaji Kituo cha Mkenda–Nakawale, kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 240.8 fedha kutoka Serikali Kuu na nyumba ya mtumishi iliyogharimu kiasi cha shilingi 133.7 zilizofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
Akizungumza katika hafla hiyo, Brigedia Jenerali Ahmed amesema maendeleo ya taifa yanategemea uwepo wa usalama imara, amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Franklin Rwezemula, akimwakilisha waziri wa mambo ya ndani amesema Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Idara ya Uhamiaji, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza ufanisi wa utendaji na kuimarisha usalama wa mipaka ya nchi
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Dkt. Lazaro Komba, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali, akibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza wa barabara ya Likuyufusi–Mkenda yenye urefu wa kilomita 60 kwa kiwango cha lami.





0 Comments