Sauti kutoka Nyikani
Na Gordon Kalulunga
NCHI yetu imepita katika vipindi kadhaa kama mwili wa binadamu, yaani kuumwa baadhi ya viungo na kupona.
Nawapongeza viongozi walioandika vitabu vya Majuto yaani wakijutia mambo waliyoyafanya wakiwa madarakani.
Nadhani hao ni Walimu Wazuri kwetu na kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ili yaliyotokea kwenye Tawala zilizopita hayapaswi kujitokeza sasa na baadae maana yakija jitokeza naye pia atatoa machozi kwenye kitabu chake kwa kujutia kuyafanya yasiyo haki katika utu na rasilimali za nchi.
Naandika huku moyo ukiniuma na sijui kwanini moyo unaniuma, lakini nadhani kwasababu hatujafika tuendako.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuapishwa alisimamisha meza yenye miguu Minne ambayo kila mguu ulikuwa na jina lake.
Meza hiyo ni falsafa yake ya 4R.
Mguu wa kwanza akauita Reconciliation, mguu wa pili unaitwa Resilience, mguu wa Tatu unaitwa Reform na mguu wa Nne unaitwa Rebuilding.
Majina hayo ya Kiingereza nitayafafanua kwa Kiswahili cha kwetu, hivyo naomba ambatana nami hapa chini.
1. Reconsiliation yaani Maridhiano.
Kama tujuavyo, Maridhiano ni muhimu na huleta matibabu.
Hakuna ubishi kwamba tulipokuwa tumefikia mioyo ya watu wengi ilioteshwa hasira ziendazo kwenye usugu zisizo nzuri, hivyo falsafa ya Rais Samia hasa neno hili la maridhaino nadhani inapaswa kuridhiwa na Watanzania kwa Umoja wetu. Tumuunge mkono kiongozi wetu.
2. Resilience yaani Ustahimilivu.
Jambo hili ni muhimu sana hasa katika nchi yetu ukizingatia sisi siyo kisiwa na tunayaona yanayotokea kwa baadhi ya nchi duniani.
Hivyo falsafa hii ya Ustahimilivu ni jambo zuri sana kwetu sote tukiongozwa na wanasiasa wa pande zote mbili, yaani chama Tawala na vyama vyenye sera mbadala.
3. Reform yaani Mageuzi.
Kwenye neno hili ni muhimu sana pia tukawa na uelewa wa pamoja na kutafsiri vema maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba Mageuzi haya hayapaswi kuwa tu yana manufaa kwa waliopewa fursa za kutafuna matunda ya Uhuru kutokana na urefu wa kamba Walizopewa.
Nadhani Maridhiano haya ni muhimu yakanufaisha vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla ikiwemo kubuni Miradi pia inayopeleka/kubakiza pesa kwa wananchi badala ya kuwa na Miradi mingi ambayo wananchi wanabaki kuwa watazamaji na kuchangia tena nguvu zao bila kubaki na chochote mifukoni kwa ajili ya kumudu maisha yao ikiwemo kununua gharama za matibabu.
4. Rebuilding yaani Ujenzi mpya.
Neno hili ni zuri sana kwetu sote na linapaswa kuungwa mkono kwa kujenga upya Taifa letu ambalo lilifikia hatua ya kuwa vipande vipande ila wengi walikuwa na wapo wanaoogopa kusema kwasababu walishuhudia yaliyompata kila aliyesema mapungufu katika taifa na Serikali.
Naamini Rais Samia wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anayo nia njema ya kujenga upya Tunu zetu za utu, umoja, udugu, maelewano, ushirikiano, pamoja na amani na kila mmoja asisimkwe kwa furaha kuishi katika Taifa letu badala ya nchi kuonekana kana kwamba ni kwa ajili ya chawa peke yao.
Akiwaapisha Mawaziri Julai 26,2024 ameendelea kuwasisitiza wasaidizi wake kuishi katika maoni yake ya falsafa ya 4R na kutambua kuwa Katiba imesema Wananchi ndiyo wenye Mamlaka na nchi, ndiyo maana ninasema kuwa Rais Samia na wasaidizi wake wakifuata Falsafa ya 4R inaweza kumwepusha kuja kuandika Kitabu cha kujutia utawala wake akistaafu.
0765615858

0 Comments