Zaidi ya wananchi 200 wa kijiji cha Kihangaiko, kata ya Msata mkoani Pwani, wamefaidika na huduma za matibabu, elimu ya afya, pamoja na msaada wa chakula uliotolewa na Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi (RTS) Kihangaiko ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano kati ya jeshi na raia wakati wa kuhitimisha zoezi la medani la wapiganaji wapya (kuruta).
Akizungumza wakati wa kutoa misaada hiyo, Mkuu wa Shule ya RTS Kihangaiko, Brigedia Jenerali Sijaona Michael Myalla, amesema huduma hizo ni sehemu ya Zoezi la Medani linalojulikana kama “EXERCISE MALIZA”. Amesema jeshi lina wajibu wa kuonyesha upendo na mshikamano kwa wananchi ambao ndio wamiliki wa jeshi hilo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Shule hiyo, Meja Edwin Mboya, amebainisha kuwa mbali na kutoa matibabu kwa maradhi mbalimbali, wametoa pia elimu ya kinga dhidi ya magonjwa ili kuwajengea wananchi uwezo wa kujilinda kiafya.
Amesema pamoja na matibabu pia walipata nafasi ya kuchunguza afya za wananchi hasa watoto na watu wazima katika kadhia mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwamo vifua, shinikizo la damu na maradi mengine
Nao wananchi na uongozi wa kijiji hicho wamelishukuru jeshi kwa moyo wa ukarimu. Mwenyekiti wa Kijiji cha Kihangaiko, Shabani Mkomo, amesema mahusiano kati ya shule hiyo na kijiji chao yamekuwa ya mfano, huku wakazi wakielezea kufurahishwa kwao na huduma ya chakula na dawa walizopata bure.
Tangu kuasisiwa kwake Septemba Mosi, 1964, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kudumisha utamaduni wa kutoa huduma za kijamii na misaada ya kibinadamu, jambo ambalo limekuwa chachu ya ulinzi wa amani na ushirikiano wa karibu kati ya jeshi na raia (Civil-Military Cooperation).




0 Comments