Na Gordon Kalulunga.
MJUMBE wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa NEC Ndugu Ndele Mwaselela ametolea ufafanuzi kauli kuhusu utaratibu maalum wa michango ya vyakula shuleni aliyoitoa Mei,28,2024 akiwa anazungumza na machifu wa Mbeya Vijijini kuelekea tamasha la kabila la Wasafwa.
Katika video upili iliyosambaa mitandaoni jana Mei 29,2024 anatolea ufafanuzi wa jambo hilo na zifuatazo ni nukuu zake.
"Zipo Kata masikini Mbeya DC, ambazo Mimi kama mdau wa elimu nimesema shule za Msingi Mbeya DC na Sekondari madarasa ya mitihani, wanafunzi wasirudishwe kwasababu ya kukosa chakula badala yake sisi kama wadau tukiongozwa na Mimi mwenyewe M-NEC, tutatafuta chakula tuweze kuwachangia katika shule hizo, huo ndiyo utaratibu tuliyousema".
"Na kwa mtu aliyeishi maisha ya chini kama Mimi, lazima nisimamie kwenye hilo. Watoto masikini wapo kidato cha pili, wapo darasa la Nne na kidato cha Nne, kipindi hiki cha mtihani wakipata msongo wa mawazo, wakisumbuliwa, hawawezi kufanya vizuri mitihani yao".
"Kwa hiyo niombe, narudia tena, Kamati ya siasa ya Wilaya ambayo Mwenyekiti nilikuwa naye na Mwenezi nilikuwa naye, wakutane na maafisa Elimu kwa kupitia Mkuu wa Wilaya, waainishe shule zenye changamoto za hao watoto, tujue idadi ya watoto, Mimi na wenzangu, tuanze kuwachangia hao watoto kwa ajili ya chakula, lakini watoto hao wasirudishwe nyumbani kwasababu ya kukosa michango ya chakula".
"Na nitoe wito kwa Watanzania, mama Samia ametoa Elimu bure, anataka watoto wasome bure kweli kweli, kwa hiyo Wazazi mkishakubaliana, siyo suala la mtoto kufukuzwa, kwasababu tunazo kesi hapa kwamba watoto wanafukuzwa na kuna baadhi nimezipeleka kwa Mkuu wa Mkoa na zingine nimemwambia Mkuu wa Wilaya, kwa hiyo siongei kwa kufikirika bali naongea kwa kumaanisha na ninazo data (takwimu).
"Lakini la pili nafanya ziara. Sisi kama wasimamizi wa Serikali Mkoa, lazima twende na dira ya Rais Samia Suluhu Hassan".
"Kwa hiyo shida hapa ni kuelewa ujumbe kuanzia mwanzo mpaka mwisho, hivyo nitoe ujumbe kwamba Mimi ni mdau wa elimu, siyo wa leo bali miaka zaidi ya 20".
"Sisi tunao watoto hapa ambao Wazazi wao wanakwama karo kabisa, hajalipa, tunawasomesha na mpaka leo ninavyoongea ninawasomesha watoto zaidi ya 65. Wapo Paradise na Patrick Mission. Wapo watoto wanasoma kuanzia awali mpaka kidato cha Sita bure".
"Lazima tuwe na huruma, hizi fedha zitaondoka lakini utu Mungu atatuuliza tulifanya nini".
"Niombe wito kwa wadau wengine tuungane na mimi nitaanzisha harambee kwa ajili ya kuwachangia hawa watoto".
Mwisho wa kunukuu.

0 Comments