Kila Wilaya wataka aende huko
Na Gordon Kalulunga
ZIARA ya Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa NEC Mkoa wa Mbeya Ndugu Ndele Mwaselela iliyokwenda kwa jina la Salaam za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mchakamchaka wa M-NEC Mwaselela katika Jimbo la Mbeya Vijijini, imezaa matunda tamanishi kwa Majimbo mengine.
Unaweza kujiuliza kwanini? Twende taratibu bila matumizi mabaya ya hasira.
Ziara hiyo ililenga kusikiliza kero za wananchi wa Jimbo hilo bila kujali itikadi za siasa na kuzitatua akiambatana na baadhi ya wataalam wa Halmashauri husika na kuleta msukumo wa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Ziara hiyo alianzia Kata ya Iwindi Juni 4, mwaka huu kisha kuelekea Kata ya Ilungu.
Akiwa Kata ya Ilungu alisikiliza tuhuma za kiasi cha Shilingi Milioni 42 za idara ya Afya na kuiwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera na kero ya kuondolewa gari la wagonjwa Ambulance katika Kituo cha Afya cha Ilungu ambapo Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo (DMO) alipopigiwa simu ili kutolea ufafanuzi alikiri na kwamba gari hilo litarejeshwa hivi karibuni katike Kata hiyo.
Katika Kata ya Igoma wananchi walimtwisha zigo la uhitaji wa Barabara ya Lami kutoka eneo la Isyonje kwenda Makete ambayo ni Barabara ya uchumi kwa wananchi hao.
Kata ya Ulenje wananchi walieleza uwepo wa shida ya Maji, M-NEC Mwaselela alijibu kero yao papo kwa papo kupitia wataalam ambao aliongozana nao.
Katika Kata ya Maendeleo kiongozi huyo aliwachangia "Bandro" 5 za bati kwa ajili ya shule shikizi na Serikali kupitia wataalam waliahidi kuanza ujenzi wa Shule ya Msingi Julai mwaka huu ambapo imetengwa Jumla ya Shilingi Milioni 600.
Pia wananchi wa Mwabowo waliahidiwa kupatiwa Barabara yenye urefu wa KM 6 chini ya Wakala wa Barabara nchini (TANROAD).
Wananchi wa Kata ya Lwanjilo wameahidiwa kupata kiasi cha Milioni 10 kwa ajili ya masuala ya Elimu.
Akiwa Ikukwa M-NEC Mwaselela alichangia Mifuko 140 ya Saruji huku akitoa maelekezo kwa serikali kupeleka Maji katika Kituo cha Afya cha Ikukwa ambacho kinafanya kazi.
Baada ya hapo akiwa anaelekea Kata ya Mjele alisimamishwa na watoa huduma za usafirishaji kwa njia ya mabasi wakimweleza kero ya vifusi ambavyo havijasambazwa kwa muda mrefu.
Hivyo aliwaelekeza wataalam kuanza kuvisambaza haraka vifusi hivyo na wataalam kutoka TANROAD kuahidi kuongeza Km 6 za ujenzi wa Barabara hiyo.
Akiwa Kata ya Mjele alichangia kiasi cha Shilingi Lakini Mbili (Tsh 200,000) kwa ajili ya chakula cha wanafunzi.
Wananchi wa Kata ya Isuto walimweleza changamoto mbalimbali ikiwemo ya Maji katika Kata hiyo ambapo alipiga Simu kwa Naibu Waziri wa Maji ambaye aliahidi kutatua changamoto hiyo kuanzia Julai mwaka huu, huku Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera pia akiwaeleza wananchi wa Isuto kwa njia ya simu kwenye Mkutano wa hadhara kuwa tatizo hilo wamelichukua kwa uzito na hivi karibuni wananchi watatabasamu.
Katika Kata ya Ilembo M-NEC Mwaselela alimpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera na kumweleza changamoto aliyoambiwa na Wananchi kuhusu kusuasua kwa Sekondari ya wasichana ya Pareto ambapo Mkuu wa Mkoa huyo aliahidi kutekeleza.
Akiwa katika Kata ya Iyunga Mapinduzi, M-NEC Mwaselela alichangia kiasi cha Shilingi Lakini Tano (500,000) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maabara ya shule ya Sekondari Mwakipesile huku akihamasisha wananchi kuungana katika Utekelezaji wa ujenzi huo.
Vivyo hivyo katika Kata hiyo wataalam kutoka serikalini waliahidi kutatua changamoto ya Maji kwa kuchimba visima Vitatu.
Akiwa Kata ya Igale wananchi walimweleza kiongozi huyo kuhusu tatizo la umeme na Maji.
Kupitia wataalam Serikali iliahidi kupeleka umeme katika Vijiji Vitatu huku mtandao wa Maji ukiongezwa KM 12.
Ikumbukwe kuwa Igale ndiko upo mradi mkubwa wa Maji ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Mbeya aliuzindua.
Kata ya Itewe kiongozi huyo alichangia tofali za Block ziparazo 2,000 kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba ya shule huku serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akiahidi kutatua changamoto ya Maji.
Haya ni baadhi ya matunda ya ziara ya Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa NEC Ndugu Ndele Mwaselela akiwa Jimbo la Mbeya Vijijini na sasa kila Jimbo linamgoja kwa hamu kwenda kupeleka msukumo wa utatuzi wa changamoto zao na kutatua mambo mengine papo kwa papo kwa michango na maelekezo.
Ndiyo maana ninasema kuwa, M-NEC Ndele Mwaselela ameamsha siasa za Mkoa wa Mbeya kupitia ziara yake hiyo.
Naomba kutoa hoja.
0765615858

0 Comments