Na Gordon Kalulunga, Mbeya
MJUMBE wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Ndugu Ndele Mwaselela amemwagiza Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Mbeya Vijijini Ndugu Akimu Sebastian Mwalupindi kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kuwachukulia hatua Walimu wote watakaohusika kuwafukuza wanafunzi shuleni wale wanaokosa michango waliyokubaliana na Wazazi wao.
Hayo ameyasema akiwa Kata ya Iwindi Juni 4, mwaka huu alipokuwa katika ziara yake Wilayani humo.
Mwaselela amesema siyo haki makubaliano ya Wazazi kuwaathiri watoto na kwamba atakayethubutu kuanzia sasa kuwafukuza wanafunzi shuleni kwa sababu ya hiyo michango itakuwa halali yao.
"Michango yote ipo kwenye Sheria, hakuna mahala popote paliposema mzazi akishindwa kuchangia mchango wa mtoto wake shuleni mtoto arudishwe, hakuna hicho kitu na michango yenu mliyokubaliana na Wazazi isiwaathiri watoto kusoma shule" amesema Mwaselela.
Amesema mzazi anayeshindwa kutekeleza makubaliano ndiye anapaswa kuwajibika siyo Mwanafunzi ambaye hata hausiki na makubaliano hayo.
Amesema amemwelekeza Mkuu wa Wilaya hiyo kuanza kuwadhibiti wale wote wanaowafukuza watoto shuleni kisa Wazazi wao kushindwa kutimiza makubaliano ya michango hiyo maana wanaofanya hayo wanawakosanisha CCM, wananchi na Serikali anayoiongoza Rais Samia Suluhu Hassan.
"Utaratibu upo wazi na hakuna waraka unaosema mzazi wa Mtoto akishindwa kulipa michango mtoto anapaswa kwenda kulala nyumbani. Watoto wasome bila vikwazo vya aina yeyote na hili ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan" amesema M-NEC huyo wa Mkoa wa Mbeya ndugu Mwaselela.
"Na ninarudia hapa nipo Iwindi, kwa Mkoa mzima, isitokee mtoto anarudishwa nyumbani kisa kukosa mchango wa aina yeyote ambao wamekubaliana wazazi" alisema Mwaselela.

0 Comments