Sauti kutoka Nyikani
Na Gordon Kalulunga
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) Ndugu Ndele Mwaselela amehitimisha ziara yake katika Jimbo la Mbeya Vijijini ambayo ililenga kuimarisha chama hicho na kutatua papo kwa papo kero za baadhi ya wananchi.
Ziara hiyo imekuwa na mitazamo KANDE kutoka kwa baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa.
Akiwa katika Kata ya Nsalala, kiongozi huyo kwa huzuni kasikika akisema kuwa Kuna dhambi inatendwa na viongozi.
Aliitaja dhambi hiyo kuwa ni viongozi kusahau maisha ya watu huku wakijisifia kwa kutajana vyeo vyao.
Kwa kuwa Kiongozi huyu ni mwakilishi wa Mkoa wa Mbeya katika kikao kikubwa cha CCM yaani Halmashauri kuu ya CCM Taifa na wanakuwa pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, natamani jambo hili akaliseme mbele ya Rais.
Naamini katika ziara yake amejionea angalau kwa kiasi fulani umasikini unaoendelea kufinyanga ngozi za sura za wapiga kura na hali ya miundombinu ya Barabara na Jiongrafia ya Jimbo husika isivyoeleweka.
Endapo kauli hii ya kusahau maisha ya watu atamweleza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ikiwezekana hadharani, Wala hatoomba makofi kutoka kwa wananchi.
Kauli pacha na hii aliwahi kuitoa Waziri wa fedha wa wakati huo ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango mbele ya Marehemu Dkt. John Magufuli kuwa licha ya ndimi zao kusema uchumi ulifika kiwango cha kati lakini Jimboni kwake wananchi wa kawaida umasikini ulikuwa unazidi.
Tutafakari masikini kuishi kama wafu huku wenye vyeo tukisemeana kwamba mambo ni poa.
Ndiyo maana ninasema kuwa, M-NEC Mwaselela kasema kweli kuhusu maisha ya watu, amfikishie mama na mifumo yetu ilivyo ya utawala na utendaji kazi wake.
Karibuni sana Nyikani ambako Kuna wakati matajiri waliishi kama mashetani na masikini kama wafu.
0765615858

0 Comments