AG JOHARI, SACP RWAMBOW, MAKAMPUNI YA ULINZI WAZUNGUMZA VURUGU ZA UCHAGUZI

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, jana Januari 15, 2026, iliendelea na mfululizo wa vikao vyake vizito jijini Dar es Salaam kwa kuwahoji mashahidi muhimu wa kisheria na usalama.

Katika vikao hivyo vilivyofanyika katika Ukumbi wa Manyara uliopo ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume hiyo awali ilikutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari baadaye  Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mstaafu wa Polisi (SACP), Jamal Rwambow, pamoja na wawakilishi wa makampuni binafsi ya ulinzi.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na namna matukio hayo yalivyoanza, athari zake kwa watu, mali na miundombinu pia ushauri wa namna ya kuondokana na matukio hayo.

Tume inaendelea kukutana na makundi mbalimbali  wakiwemo waathirika wa Matukio hayo lengo ni kupata  kiini cha chanzo cha matukio hayo na kuyawasilisha kwa ajili ya hatua zaidi.


Hadi sasa, Tume inaendelea na utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali, yakiwemo ya waathirika wa moja kwa moja wa machafuko hayo, lengo likiwa ni kupata kiini cha chanzo cha matukio hayo. Ripoti itakayotokana na ushahidi wa makundi haya inatarajiwa kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kiserikali.


Vikao hivi ni sehemu ya mchakato mpana wa maridhiano ya kitaifa uliotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ukilenga kuiponya nchi na kurejesha amani ya kudumu baada ya msukosuko wa uchaguzi wa mwaka jana. Tume imewahakikishia wadau wote kuwa kila ushauri na ushahidi unaotolewa unazingatiwa kwa uzito mkubwa ili kuleta suluhu ya kudumu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment

0 Comments