Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa ujumbe mzito kwa washirika wa kimataifa na wakosoaji wa demokrasia nchini, akisisitiza kuwa Tanzania ni taifa lililoanza mchakato wa ndani wa "kujiponya na kujirekebisha" (internal healing and self-correction) bila kuhitaji shinikizo la nje.
Akihutubia mabalozi katika hafla ya Sherry Party Ikulu Chamwino, Rais Samia ameweka wazi kuwa serikali yake inatambua changamoto zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, lakini akasisitiza kuwa changamoto hizo ni sehemu ya safari ya kuelekea ukomavu wa kisiasa.
"Demokrasia ni Safari, si Tukio" "Mataifa yote duniani, hata yale yaliyostawi, yana changamoto zao za kisiasa. Kinachotutofautisha ni ujasiri wa kukabiliana na makosa yetu," alisema Rais Samia. Kwa kuzungumzia msamaha wa wafungwa 1,787 na kuahidi kuunda Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC), Rais ametuma ujumbe kuwa Tanzania ina mifumo thabiti ya ndani ya kutatua migogoro.
Rais alifafanua kuwa mchakato wa Katiba Mpya sasa unapewa kipaumbele si kwa sababu ya shinikizo, bali kama hitaji la lazima la kijamii ili kuunganisha taifa. "Tunajirekebisha sisi wenyewe kwa sababu tunajipenda, na tunajua tunakokwenda. Tunawaomba washirika wetu kuheshimu mamlaka yetu (sovereignty) wakati tukipita kwenye kipindi hiki cha mageuzi," alisisitiza.
Ujumbe wa 'Repair, Rebuild, Renew' Falsafa yake ya muhula wa pili—Kukarabati, Kujenga Upya, na Kufanya Upya—imepokelewa kama mwongozo wa kidiplomasia unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki. Rais amewataka mabalozi kutathmini Tanzania kwa mwelekeo wake wa baadaye badala ya matukio ya mpito yaliyopita.
Uchumi Shindani: Muhuri wa Fitch na Moody’s
Ili kuonyesha kuwa utulivu wa kisiasa una maana ya kiuchumi, Rais amewasilisha ripoti ya kishindo ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) wa asilimia 5.9. Tanzania sasa imevunja rekodi yake yenyewe kwa kusajili miradi 927 ya uwekezaji ndani ya mwaka mmoja pekee, ikiwa na thamani ya Dola bilioni 11.09.
Imani ya dunia kwa Tanzania imethibitishwa na ripoti za mashirika ya kimataifa ya Moody’s (B1) na Fitch (B+), yaliyotoa alama ya "Stable Outlook" (Mwelekeo Thabiti). Hii inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazokopesheka kwa urahisi na zenye mazingira salama ya biashara.
Lango la Biashara
Rais pia alizungumzia Dira ya Maendeleo ya 2050, lengo likiwa ni kufikia uchumi wa Dola trilioni 1, alisema kwamba Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha huduma (Service Hub):
Miundombinu (TAZARA & SGR): Kwa msaada wa Dola bilioni 1.4 kutoka China kwa ajili ya TAZARA, na kukamilika kwa SGR ifikapo Julai 2026, Tanzania inakuwa lango kuu la biashara kwa nchi za SADC na EAC.
Diplomasia ya Matibabu (Medical Diplomacy): Rais ametangaza mkakati wa kuitumia hospitali kama JKCI kuvutia utalii wa matibabu, huku taifa likizindua Pharmaceutical Investment Acceleration Programme kwa ajili ya viwanda vya dawa.
Nishati Safi (Green Diplomacy): Tanzania imejipanga kutumia soko la kaboni (Carbon Credit Market) na nishati ya kupikia ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi, ikiitaka dunia kutoa teknolojia badala ya ahadi.
Tanzania Inayotazama Mbele
Rais Samia akimnukuu Søren Kierkegaard, anasema, "Maisha yanaeleweka kwa kutazama nyuma, lakini yanaishi kwa kutazama mbele," Rais Samia amewahakikishia mabalozi kuwa Tanzania imejifunza kutokana na makosa ya nyuma na sasa inapiga hatua kuelekea kwenye haki, mazungumzo, na ustawi wa kiuchumi usio na kikomo.

0 Comments