Tanzania imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu na mlezi wa amani katika Ukanda wa Maziwa Makuu, kufuatia hatua ya serikali kuanzisha mabadiliko ya kimkakati katika usimamizi wa kambi za wakimbizi nchini ili kuimarisha ulinzi wa ndani na ustawi wa kijamii.
Msimamo huo umejitokeza Januari 19, 2026, jijini Dodoma, wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi na Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Leontine Nzeyimana. Mazungumzo hayo yamelenga namna mataifa haya mawili yanavyoweza kushirikiana kudhibiti uhalifu na kutoa elimu kwa wakimbizi, ikiwa ni sehemu ya ulinzi wa ndani wa mipaka ya Tanzania.
Akielezea umuhimu wa kikao hicho, Waziri Katambi amesisitiza kuwa Tanzania haitoi tu hifadhi, bali inatekeleza jukumu lake kama mlezi wa amani kwa kuhakikisha kuwa kambi za wakimbizi hazitumiwi kwa vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi jirani au kuvuruga utulivu wa ndani wa Tanzania.
"Tunafanya mabadiliko ya kimkakati katika utoaji wa elimu na udhibiti ndani ya kambi hizi. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa jamii ya wakimbizi inaishi kwa ustawi na nidhamu, huku tukidhibiti mianya yote ya uhalifu ambayo inaweza kuathiri usalama wa raia wetu na mali zao," alibainisha Waziri Katambi.
Mabadiliko hayo ya kimkakati yanatazamwa kama hatua ya kisasa ya usimamizi wa wakimbizi, ambapo serikali haishughulikii tu mahitaji ya dharura, bali inawekeza katika mifumo ya elimu na malezi ya kijamii ili kuandaa mazingira salama kwa wakimbizi kurejea makwao kwa hiari na sifa njema pindi hali itakaporuhusu.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, kinaashiria muingiliano wa kidiplomasia na usalama unaolenga kuifanya kanda hii kuwa na amani ya kudumu.
Kwa hatua hii, Tanzania inatuma ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa inaendelea kuwa mlinzi wa tunu za amani, huku ikijidhatiti kulinda usalama wa mipaka yake kupitia mipango madhubuti na ushirikiano wa karibu na nchi jirani.

0 Comments