Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ameweka wazi kuwa mustakabali wa maendeleo ya kiuchumi nchini unategemea kwa kiasi kikubwa namna jamii inavyowekeza katika malezi bora ya watoto yenye kujenga nidhamu, uvumilivu, na uwajibikaji.
Akifungua Maonesho ya 32 ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ya Nanenane Kanda ya Kaskazini katika Viwanja vya Themi-Njiro jijini Arusha, alionya kuwa baadhi ya mifumo ya kisasa ya malezi inayowapa watoto kila wanachokitaka bila kuwafundisha kufanya kazi kwa bidii inachangia wimbi la vijana kukosa subira.
Alisisitiza kuwa wazazi na walezi wanapaswa kutafakari kwa kina nafasi yao katika kuandaa kizazi chenye uzalendo na uwezo wa kukabili changamoto za maisha ili kulinda nguvu kazi ya taifa na kuepusha tabia hatarishi kama uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya.
Sambamba na suala la maadili, Naibu Waziri Silinde alisisitiza umuhimu mkubwa wa kulinda amani na utulivu akibainisha kuwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni kitovu cha kipekee cha sekta ya utalii, biashara, na uwekezaji ambayo inategemea usalama ili kustawi.
Alionya kuwa vurugu au uvunjifu wowote wa amani utaangusha uchumi wa wananchi wengi wanaotegemea sekta hiyo kupitia kupotea kwa watalii na kudorora kwa biashara.
Aidha aliwataka wananchi wote kuimarisha ushirikiano wao na vyombo vya dola kwa kulinda usalama wa nchi, hususan wakati huu Tanzania inapojiandaa kwa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), akihitimisha kuwa ulinzi wa amani ni wajibu wa kila mmoja kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.
0 Comments