Safari ya Kwenda 2050: Hivi Ndivyo Tanzania Inavyojipanga Kuwa Giant wa Kiuchumi na Viwanda Barani Afrika!

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka bayana vigezo vya kuchagua sekta za kimkakati za kuchochea mageuzi ya kiuchumi, ikisisitiza kuwa sekta za kipaumbele lazima ziwe na uwezo wa kujizalishia ajira zenyewe, kuchochea ukuaji katika sekta nyingine, na kuunganisha soko la ndani na la nje kupitia uongezaji thamani wa bidhaa na malighafi. 

Ili kufikia malengo hayo, uchumi wa Tanzania unatazamiwa kujengwa kupitia nguzo kuu za sekta za uzalishaji viwandani, kilimo cha kisasa, fedha, uchumi wa buluu, utalii, madini, huduma, ujenzi na milki, pamoja na michezo na ubunifu.

Sekta ya viwanda inatarajiwa kupanuka na kuwa msingi mkuu wa uchumi ifikapo mwaka 2050, ikilenga kufanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vyenye ushindani wa kimataifa kwa kuimarisha miundombinu, sera, ujuzi na upatikanaji wa mitaji. 

Sambamba na hilo, kilimo ambacho bado ni mhimili mkuu wa uchumi kikichangia ajira na pato la taifa, kitapitia mabadiliko makubwa kupitia uwekezaji katika zana za kisasa kama matrekta na vituo jumuishi vya kilimo, mifugo, uvuvi, na misitu ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha chakula barani Afrika.

Sekta ya fedha nayo itaimarishwa ili kurasimisha shughuli za kiuchumi na kuongeza upatikanaji wa mikopo, wakati rasilimali za bahari na maziwa zitatumika kikamilifu kupitia uchumi wa buluu kuongeza ajira na mapato.

Ukuaji wa uchumi pia utaungwa mkono na sekta ya utalii inayochangia fedha za kigeni, ambayo itapanuliwa zaidi kupitia utalii wa mikutano, fukwe, utamaduni, na mazingira, wakati sekta ya madini itajikita katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya rasilimali hizo nchini.

Aidha, sekta za huduma, ujenzi na milki zitaimarishwa ili kukidhi mahitaji ya miji inayokua na kuongeza ajira kwa wataalamu wa nyanja mbalimbali. Mwisho, sekta ya michezo na ubunifu itapewa kipaumbele ili kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana na kuitangaza Tanzania kimataifa katika muziki, filamu, sanaa, na michezo ifikapo mwaka 2050.

Post a Comment

0 Comments